Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi za serikali Mpwapwa zadaiwa bili za milioni 197.5/-

D9c4d22c6ba96dddd8dfd2d119597c93 Taasisi za serikali Mpwapwa zadaiwa bili za milioni 197.5/-

Wed, 16 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mpwapwa (MPWUWSA) inazidai taasisi mbalimbali za serikali wilayani humo madeni ya ankara za maji yanayofi kia Sh milioni 197.5.

Akitoa ripoti kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri alisema mamlaka hiyo inaendelea kufuatilia taasisi hizo ili zilipe deni hilo.

“Mamlaka kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya na wizara ya maji tunaendelea kufuatilia taasisi za serikali ili zilipe madeni hayo,” alisema.

Shekimweri alisema katika kukomesha madeni yasiendelee kuongezeka, Mpwuwsa inatarajia kuanza kuzifungia taasisi na wateja husika mita za malipo kabla ili kudhibiti ongezeko la madeni hayo.

Alisema baadhi ya taasisi ambazo ni watumiaji wa maji hawalipi huduma hiyo kwa wakati na nyingine hazilipi kwa kipindi kirefu na hivyo taasisi hiyo inashindwa kulipa gharama za umeme ambazo taasisi hizo inadaiwa na Tanesco.

Alisema katika kutekeleza mradi wa maji wilayani humo pia mamlaka hiyo inapambana na changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika vyanzo baadhi vya maji wilayani humo.

Pia kuna changamoto ya uharibifu wa vyanzo vya maji baridi katika eneo la Mayawile, unaofanywa na wakazi wa Kiboriani, Chaladinde na Mapinduzi na hivyo kusababisha kupungua uzalishaji wa maji ya asili kila siku.

Pia kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji isiyoendana na uongezeko la watu katika mji, kwani mji huo pamoja na mitaa yake inapanuka kwa kasi wakati huduma ya maji haiendani na kasi hiyo.

Changamoto nyingine ni kukatika kwa umeme mara kwa mara ambako kusababisha mitambo ya maji kushindwa kusukuma maji ili kuwafikia wateja. Shekimweri alisema pamoja na changamoto hizo, katika kuongeza kiwango cha maji, mamlaka hiyo inaendelea kufanya utafiti wa vyanzo vya maji chini ya ardhi katika eneo la Mji Mpya na Kikombo wilayani humo.

Shekimweri alisema utafiti huo unaofanyika, unalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 69 hadi asilimia 98 na mji huo kuwa uhakika wa upatikanaji wa huduma maji.

Pia kutokana na gharama za nishati ya umeme kuwa kubwa, mamlaka hiyo imekuwa ikiomba mabadiliko ya bei za huduma kwa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ili bei za huduma ziende sambamba na gharama halisi za uendeshaji.

“Pia inaendelea kutekeleza mpango wake wa kudhibiti maji yasiyolipwa ili kuhakikisha wanapata mapato makubwa kutoka makusanyo ya Sh milioni 30 kwa mwezi za sasa na kuongezeka ambazo asilimia zaidi ya 40 zinatumika kugharamia umeme wa kuendesha mitambo,” alisema.

Katika kulinda na kutunza mazingira, mamlaka hiyo pia imekuwa ikipanda miti rafiki wa mazingira kwa kila mwaka kwa ajili ya utunzaji wa vyanzo vya maji ikishirikiana na wakala wa misitu na kusimamia utekelezaji wa sheria ya mazingira.

Kuhusu kukatika kwa umeme, mamlaka hiyo pia imekuwa ikiwasiliana na uongozi wa Taneso ili kuona namna gani wanaweza kuondoa tatizo la umeme kukatika.

Mpwuwsa iliyoanzishwa Julai mosi 2003 inahudumia kata tatu za mjini hapo za Mpwapwa Mjini, Vingh’awe na Mazae na mitaa ya Mjini Kati, Vingh’awe, Hazina, Majengo, Kota, Kikombo, Kikombo Road, Ng’ambo, Igovu, Mwanakianga, Mji Mpya, Mazae na Ilolo.

Mamlaka hiyo yenye jumla ya wateja 3,380 zikiwamo taasisi 76, wafanyabiashara 27, vioski 18 na wateja wa majumbani 3,259, inazalisha maji kutoka katika vyanzo sita. Kati ya hivyo vinne ni visima virefu na viwili ni maji mtiririko

Chanzo: habarileo.co.tz