Dodoma. Licha ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma inakabiliwa na upungufu wa watoa huduma ya afya.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa Wilaya hiyo, Saimon Odunga wakati akipokea vifaa mbalimbali, zikiwemo baiskeli, buti za mvua na majaketi vyenye thamani ya Sh10milioni vilivyotolewa na taasisi ya Mkapa Foundation kwa ajili ya watoa huduma 35 lengo likiwa ni kuwawezesha kuifikia jamii.
Amesema sekta ya afya wilayani humo ipo katika hali mbaya na inahitaji msukumo.
Amesema Wilaya ya Chemba ina watumishi 188, wanaohitajika ni 831, “tuna upungufu wa asilimia 77 ya watumishi. Tunapaswa kuboresha sekta ya afya, hata kama tutakuwa na miundombinu mizuri kiasi gani lakini watumishi ndio jambo la msingi kwa sababu wananchi wanataka kupata huduma bora,”
Mtoa huduma katika kijiji cha Itilikwi, Fatuma Mtilika amesema ukosefu wa elimu ya uzazi wa mpango umesababisha wanawake wanaoishi vijijini kuzaa bila kufuata uzazi wa mpango.
Kwa upande wake meneja wa vipindi wa taasisi ya Mkapa Foundation, Dk Adeline Nyamwihura amesema taasisi hiyo kupitia mradi wake wa Mkapa Fellows awamu ya tatu, imeanza utekelezaji katika wilaya ya Chemba kwa kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya Wilaya.
“Wameshaajiriwa na wapo hapa kwa ajili ya kupokea vitendea kazi. Kwetu ajira hii ni muhimu na ndio maana tunaunga mkono azma ya Serikali kuhakikisha kuna kiungo kati ya jamii na vituo vya kutolea huduma,” amesema Dk Adeline.
Amesema lengo la kuwatumia wahudumu hao wa afya inatokana na vifo vya wajawazito kuendelea kutokea maeneo mengi, wahudumu hao watawafikia wajawazito wanaochelewa kufika katika vituo vya afya.