Jumla ya taa 25 za barabarani zimegongwa na kuharibiwa katika matukio ya ajali barabarani zilizotokea maeneo tofauti mkoani Tabora katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Tabora, Kaimu meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani humo, Raphael Mlimaji amesema ajali hizo zimeisababishia wakala huyo hasara ya zaidi ya Sh80 milioni.
‘’Kati ya taa 25 zilizogongwa na kuharibiwa, ni taa tisa pekee ndizo wahusika wamelipa fidia baada ya kufahamika kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema walioshuhudia ajali hizo,’’ amesema Mlimaji
Pamoja na matukio ya ajali, Kaimu meneja huyo wa Tanroads ametaja wizi na uharibifu wa miundombinu ya barabara kuwa miongoni mwa matukio yanayosababishia hasara Serikali inayotumia mamilioni ya fedha kuboresha miundombinu hiyo.
‘’Tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali na taasisi zake pindi wanaposhuhudia uharibifu wowote wa miundombinu katika maeneo yao; kwa sasa, wananchi wengi hawatoi ushirikiano pindi wanaposhuhudia uharibifu wa mali za umma ikiwemo miundombinu ya barabara,’’ amesema Mlimaji
Kutokana na taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amewaagiza wakuu wote wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha ulinzi na usalama wa miundombinu ya barabara katika maeneo yao kwa kuwachukulia hatua wote wanaobainika kufanya uharibifu.
‘’Uharibifu wa miundombinu ya barabara siyo tu inaitia Serikali hasara, bali pia inahatarisha usalama na maisha ya watumiaji wa barabara kwa kukosekana kwa alama muhimu za usalama ikiwemo taa na vibao vya kuelekeza na kuhadharisha madereva na watumiaji wengine wa barabara,’’ amesema Dk Burian
Amesema juhudi za Serikali za kuongeza bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara hazitakuwa na maana iwapo watu wachache wataendelea kuachiwa kuharibu miundombinu hiyo bila kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Ametoa mfano wa ongezeko la bajeti ya fedha za barabara kupitia Tanroads na Tarura Mkoa wa Tabora kutoka Sh33.8 bilioni mwaka wa fedha wa 2020/21, Sh54.7 bilioni mwaka wa fedha 2021/22 na Sh61.9 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni ishara ya uthabiti wa Serikali katika maboresho ya miundombinu ya barabara mkoani Tabora ambazo ni lazima ziungwe mkono kwa kulinda miundombinu hiyo.
Hoja ya kulinda miundombinu ya barabara na miradi yote ya maendeleo imeungwa mkono na Rajab Mohamed, mkazi wa mtaa wa Stendi mjini Tabora akisema ni jukumu la kila raia mwema kuwadhibiti wote wanaoiharibu kwa njia moja au nyingine.