Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TUONGEE KIUME: Wanawake si wabaya, ila wana gundu

48336 Pic+wanawake

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kabla ya mwaka 1990, Richard Mason, tajiri wa Uingereza alifunga pingu za maisha na Kate. Kwa mujibu wa imani yake kipindi kile, yale yalikuwa ni maamuzi yaliyotukuka na yenye kutii maelekezo ya Mungu ya jinsi gani tunapaswa tuishi kabla ya kuondoka hapa duniani.

Mwaka 1996 wakapata mtoto wa kwanza wa kiume, wakamuita Willem. Kisha Willem alipofikisha miaka 4, hiyo ikiwa ni mwaka 2000, Kate akabeba ujauzito mwingine na alipojifungua ilikuwa ni mapacha wawili wa kiume, Ed na Joel.

Willem, mtoto wao wa kwanza, alipofika umri wa kuanza shule, Richard akamega kipande cha utajiri wake, akalipa ada ya mtoto katika shule ya bei mbaya ambayo sio kila baba ana ubavu wa kumpeleka mwanae huko — mtoto akaanza shule. Huku Ed na pacha wake Joel wakipelekwa hospitali nzuri kila walipoumwa, wakilala kitanda poa kwa jasho la baba na walikula na kusaza kwa unga uliopatikana kwa nguvu ya baba — mwanaume alijitoa kwa watoto wake.

Kisha mwaka 2007, jini mkata kamba, shetani ibilisi akavamia ndoa yao. Agano likashindwa kufanya kazi, pingu zikakatika vipande viwili. Richard akashika hamsini zake, Kate akanyanyuka na za kwake — wakatalikiana.

Richard akaoa mwanamke mwingine. Lakini ubaya ni kwamba ndoa hii mpya haikuleta matunda; yaani mtoto.

Richard na mkewe mpya wakaenda hospitali. Huko daktari akamweleza Richard kuwa ana ugonjwa wa kurithi wa Cystic Fibrosis. Ugonjwa ambao kwa kawaida — wanaume wote wenye nao, hawawezi kusababisha mimba kwa mwanamke.

Maana yake ni nini? Kama ni ugonjwa wa kurithi, Richard hakutakiwa kuwa baba wa watoto wake labda tu kama Mungu aliamua kufanya miujiza ya kuwashangaza madaktari.

Lakini Richard hakuwa na imani ya ajabu kiasi hicho. Akawaamini madaktari na alichokifanya ni kumfungulia kesi mke wake wa zamani. Ambapo mahakamani, Kate alikiri kuwa kweli watoto wote watatu hawakuwa wa Richard. Akamlipa fidia lakini akaomba kutomuweka wazi baba wa damu wa watoto wake.

Kwa hiyo, muda na kila kitu alichokitoa Richard kwa wale watoto watatu aliozaa na Kate kabla ya kuachana nae, ilikuwa anasaidia kulea damu ya mtu mwingine akiamini ni damu yake.

Kama baada ya kusoma umeelewa kuwa kisa hiki kinamaanisha kwamba wanawake sio watu wazuri, unakosea. Wanayoyafanya wanawake tunayafanya.

Tuna wanawake wengine mbali na wake zetu, tuna watoto nje ya ndoa zetu na wake zetu hawafahamu. Isipokuwa wanawake wana damu ya kunguni, kimjini mjini tunaita gundu. Wanapofanya, tatizo linaoneka kubwa kuliko kawaida, na wanaonekana ndio chanzo.

Hata wakati wa kula tunda pale edeni, Hawa alidanganywa, akala, kisha akamfuata Adam, akamdanganya, naye akala, lakini kosa linaonekana la Hawa ilihali Adam alikuwa na akili timamu, alikuwa na haki na nguvu ya kukataa na kufuata maagizo ya Mungu

Haya mambo ya duniani ni mazito sana. Tumuombe Mungu atusaidie na tumkabidhi ndoa zetu azisimamie.



Chanzo: mwananchi.co.tz