Tatizo la uoungufu wa mashuka na vyandarua katika wodi ya wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ya Bitimba imepungua baada ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Mwanza kutoa msaada wa mashuka 128 na vyandarua 128 kwa hospitali hiyo.
Pamoja na mashuka na vyandarua, TRA pia imetoa msaada wa pampasi kwa ajili ya watoto, vipima joto, viti mwendo, miswaki, dawa za meno na vifaa vya usafi, vyote vikiwa na thamani ya Sh6 milioni.
Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Ernest Dundee amesema misaada hiyo iliyotolewa Jumatatu ya Desemba 4, 2023 ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazofanyika kuadhimisha Wiki ya Mlipa Kodi
Akipokea msaada huo, kaimu mganga mfawidhi Hospitali ya Butimba, Dk Masama Lugwisha ameushukuru uongozi wa TRA kwa msaada wa mashuka na vyandarua akisema umewezesha kila kitanda hospitalini hapo kuwa na uhakika wa kupata angalau shuka na chandarua kwa siku.
Hospitali hiyo ya wilaya inahudumia wagonjwa 350 mpaka 400 wa nje kwa siku na ina uwezo wa kulaza wagonjwa 80 mpaka 100 kwa siku.
“Tunashukuru kwa msaada wa vifaa hivi ambavyo vitasaidia kuhudumia wagonjwa wanaolazwa hapa, sasa karibu kila kitanda kitakuwa na shuka na chandarua chake,’’ amesema Dk Lugwisha
Hamisa Hamad, mmoja wa wazazi waliokutwa katika wodi la wazazi, ameushukuru uongozi wa TRA kwa msaada huo akisema utawasaidia wanaoajifulia hospitalini hapo kuwakinga watoto wao dhidi ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa Malaria.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Edina Mwesiga, muuguzi katika wodi ya wazazi akisema msaada uliotolewa siyo tu umepunguza upungufu wa vifaa, bali pia utasaidia kuimarisha hali ya usafi wodini na hivyo kuepuka wagonjwa, ndugu na jamaa wanaofika hospitalini hapo na magonjwa ya kuambukiza.