Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRA, wafanyabiashara Morogoro wateta kuhusu ulipaji kodi

Tra Pic Data TRA, wafanyabiashara Morogoro wateta kuhusu ulipaji kodi

Tue, 12 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Morogoro. Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA) imetakiwa kulinda mitaji ya wafanyabiashara walipa kodi kwa kudhibiti biashara holela zisizolipiwa kodi zinazofanana na zile wanazozifanya.

Wafanyabiashara mkoani Morogoro wametoa wito huo walipokutana na uongozi wa TRA wakati wa kikao cha pamoja cha kujadili masuala mbalimbali yakiwemo ya elimu ya mlipa kodi.

Licha ya kupongeza elimu ya kodi, mijadala na ushirikiano toka kwa Meneja wa TRA Mkoa huo, Emmanuel Maro wafanyabiashara hao walishauri mambo mbalimbali kufanyiwa kazi ikiwemo juu ya namna maafisa wa TRA wanavyowakamata kwa kushtukiza wanapofika katika biashara zao kwa madai ya kutotoa risiti za mashine ya EFD.

Kiongozi wa wenye hoteli Mkoa wa Morogoro, Gregory Mtalu amesema ni vyema Mamlaka hiyo ikaendelea kutoa elimu mara kwa mara wanapofika maeneo yao ya biashara badala ya kuwaza kuwalipisha adhabu jambo ambalo linaweza kuua biashara zao.

“Kuna suala la utoaji risiti linapaswa lifanywe na wote kwa pamoja baina ya mteja na muuzaji kwani muuzaji bidhaa huenda akasahau kwa kupitiwa lakini mteja akidai anaweza kusaidia risiti kutolewa bila wasiwasi wowote, akigoma kutoa hapo ni tatizo jingine”amesema Mtalu.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Morogoro, Muadhini Myanza ameiomba Mamlaka hiyo kupunguza bei ya (uuzaji) wa mashine ya EFD kwa wafanyabiashara wadogo ili kuweza kumudu kununua mashine hizo.

Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo licha ya kutoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na wafanyabiashara hao alihimiza umuhimu wa wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati, kudai na kutoa risiti, usajili wa magari ya biashara na umuhimu wa kujisajili magari wanayonunua kwa majina yao.

Pia, Kayombo aliwasisitiza wafanyabiashara kuacha kushiriki katika udanganyifu kwa kupokea risiti zisizo na fedha halali ya manunuzi jambo ambalo litawafanya kuingia kwenye udanganyifu ambao ni kosa kisheria.

“Upo udanganyifu unatokea mtu ananunua bidhaa ya Sh2 milioni anakabidhiwa risiti ya 200,000 na ukiichukua na kuondoka nayo bila kuhakikisha risiti hiyo, utakapokamatwa kwenye ukaguzi adhabu lazima itawakuta wote wawili,” amesema.

Kayombo amekemea tabia ya watu wasio waaminifu wanaoingiza magari kinyemela na kuyauza mitaani bila kufanya mabadiliko ya umiliki na kuleta shida kwa mnunuzi baadae jambo linalosababishwa na ukwepaji wa malipo ya kodi ambayo hata hivyo alisema ni kidogo.

Amesema zoezi la ukaguzi la TRA linaanza kufanyika mwezi huu ambapo amewataka wafanyabiashara kubadilika na kujiepusha na adhabu zitakazotolewa zilizopo kisheria.

Kaimu meneja TRA Mkoa wa Morogoro Emmanuel Maro amesisitiza utoaji wa risiti kwa wafanyabiashara hasa wenye sehemu za burudani hasa kwenye matamasha ya usiku.

Aidha Maro amewataka wafanyabiashara kutumia mashine hizo katika maeneo ya biashara yao kwani kufanya hivyo kutafanikisha ukusanyaji wa mapato kwa uhakika zaidi.

Chanzo: mwananchidigital