Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPA yafuta tozo za Makasha Bandari ya Mtwara

Mtwaraport TPA yafuta tozo za Makasha Bandari ya Mtwara

Wed, 27 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini, Erick Hamis, amesema wamepunguza gharama za tozo kiasi cha asilimia 30 kwa meli zote zitakazofanya kazi ya usafirishaji wa korosho kutoka Bandari ya Mtwara kwa msimu huu wa korosho kwa ajili ya kutoa unafuu kwa wasafirishaji wa zao hilo.

Mbali na kupunguza tozo za shughuli zote za bandari, Hamis amesema pia wamefuta ushuru wa kuhifadhi makontena bandarini hapo kwa msimu mzima wa ununuzi na usafirishaji wa korosho katika bandari hiyo.

Hamis ametoa kauli hiyo jana mkoani Mtwara mara baada ya kikao cha pamoja kati yake na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,wanunuzi wa zao la korosho pamoja na wasafirishaji wa zao hilo.

Amezitaja tozo zilizopunguzwa kuwa ni  punguzo la tozo za Stevedoring kutoka dola 90 hadi 63 kwa kasha la futi 20, kutoka dola 135 hadi 94.5 kwa kasha la futi 40, sawa na punguzo la asilimia 30.

Punguzo zingine ni pamoja na  tozo za Shore handling kutoka dola 90 hadi dola 63 wa kasha la futi 20 na dola 135 hadi 94.5 kwa kasha la futi 40, sawa na punguzo la asilimia 30.

Katika punguzo hizo, Hamis amesema kuna punguzo la tozo aridhia (wharfage charges) kutoka dola10.552 kwa tani kwenda 5.276 kwa tani sawa na asilimia 0.5 ya Mali Pwani (Free On Board).

 "Hatutatoza makasha matupu ya  kuyahifadhi (storage charges) kwa msimu wa mwaka 2021/22 na hivyo kutoa unafuu wa dola 3.95 kwa siku kwa kasha,huku  Muda wa makasha yenye mzigo (Loaded/Laden Containers) kukaa bandarini bila tozo ya kuhifadhi itakuwa ni  siku kumi na tano  hivyo  hali inayofanya tuwe tmeondoa gharama ya dola 19.8 kwa kila siku inayoongezeka sawa na jumla ya dola 158.4 kwa siku 8." amesema Hamis

Ameeleza kuwa mbali na tozo hizo pia Mamlaka ya Bandari imetoa kipaumbele kwa  meli zinazotoka Mtwara kuegeshwa Bandari ya Dar es  Salaam  ndani ya saa 24 na pasipo gharama hivyo kupunguza gharama za uendeshaji kwa wenye meli ambazo zinakadiriwa kuwa kati ya dola 15,000 hadi dola 30,000 kwa siku.

Awali Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watumiaji wa bandari ya Mtwara hasa kwa msimu huu wa korosho kwa ajili ya kumpunguzia gharama za uendeshaji msafirishaji pamoja na mkulima wa zao la korosho.

Ameongeza kuwa uamuzi wowote unaofanywa na serikali unahakikisha unalinda maslahi ya wakulima,wanunuzi na wasafirishaji.

"Wanunuzi msihofu kushindana kwenye bei ya kununua korosho wala msitoe bei ya chini shindaneni kwa haki kwa kuwa kila kitu kinaenda sawa na kwa sasa tumeshakuwa na uhakika wa kupata makontena zaidi ya 6000 yatakayokuja muda wowote kuanzia sasa"amesema Bashe.

Chanzo: ippmedia.com