Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi wa Wilaya ya Makete mkoani Njombe kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga baridi ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na hali hiuyo.
Meneja wa kituo kikuu cha Utabiri cha TMA, Samwel Mbuya amesema hali ya baridi katika wilaya hiyo na maeneo mengine ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeongezeka.
Alipoulizwa kuhusu video inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii inayoonyesha hali ya baridi na theluji ikidai kuwa eneo hilo ni moja ya eneo la Makate, Mbuya amesema taarifa hizo wameziona na huenda ikawa ni sahihi.
“Taarifa hizo kweli zipo tumeziona, lakini kipindi hiki kwenye kipupwe ni hali ya kawaida kwa maeneo hayo lakini kinochoonekana sio theluji bali ni umande” amesema
Amesema kwa siku mbili sasa baridi imeongezeka katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za juu kusini hivyo wananchi waendelee kuchukua tahadhari.
Amesema Mamlaka imefuatilia video hiyo hali hiyo inayoonekana inaweza ikawa halisi ingawa sio theluji kama baadhi wanavyodhani.
Mbuya amebainisha hali hiyo kwa maeneo ya Makete ni kawaida hasa kwa vipindi vya kipupwe ingawa kila mwaka hali inatofautiana.
Amebainisha kuwa kwa siku mbili kuanzia jana Jumanne hali ya baridi katika eneo la Makete ni kati ya nyuzi joto sita hadi nane (6-8°C)
Mkurugenzi huyo amesema kuwa hali hiyo ni umande unaotokea baada ya mgandamizo wa ardhi na baridi.
Amesema hali hiyo ambayo kitaalamu inaitwa Sakitu ni umande ulioganda kutokana na baridi kali, inayoonekana kama tabaka jembamba la theluji linalofunika mimea, miti na vitu vyingine.
Amewataka wananchi wa maeneo hayo kuendelea kuchukua tahadhari za kawaidi za kujikinga na baridi ikiwa ni pamoja na kuvaa nguo nzito.
Pia, ameshauri kuendelea kufuatilia ushauri wa wataalamu wa afya pamoja na wataalamu wa kilimo.
Hata hivyo, hali hiyo ya baridi kwa sasa haijafikia kiwango cha chini ambacho Mamlaka hiyo ilitabiri wakati ikitoa mwelekeo wa mwelekeo wa kipupwe kwa mwezi Juni hadi Agosti 2022.
Wakati akitoa mwelekeo wa kipupwe wa kipindi hicho katika mikoa mitano ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi yenye miinuko, Mkurugenzi wa Huduma za Utafiti na Matumizi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a alisema hali ya baridi inatarajiwa kuwa kali chini ya nyuzi joto nne (4 °C)
Alisema kiwango cha baridi katika maeneo hayo kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 4 hadi 14, huku maeneo yenye miinuko yakitarajiwa chini ya nyuzi joto nne.
Wananchi wazungumza
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wananchi kutoka baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Kusini wamesema hali hiyo inawatesa hivyo wanatumia njia mbadala kuongeza joto.
Ofisa ufuatiliaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Wilaya ya Makete, Heri Mpunza amesema “Hali ni mbaya, baridi ni kali. Mimi binafsi natumia hita kwaajili ya kuongeza joto chumbani lakini wakati wa kutoka nyumbani kwenda kwenye majukumu baridi ni kali.”
“Shida kwa wanafunzi, ingawa wengi wanaingia shuleni saa mbili asubuhi shuleni lakini wanateseka. Kuna muda ukiwa unaendesha gari ukungu unatanda hauoni,” amesema
Mkazi wa Makete, Neema Francis amesema yeye anatumia mkaa kujinusuru na hali hiyo hasa wakati wa usiku.
Neema alipoulizwa kama haoni kuwa ni hatari kutumia njia hiyo, amekiri kuwa pamoja na njia hiyo kuwa hatarishi lakini inamsaidia yeye na familia yake.
“Kweli baridi ni kali na ukiwaona watoto asubuhi utawaonea huruma, mimi ninachofanya ni kuwasha mkaa kwenye kupata joto”