Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa angalizo la uwapo wa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi, zitakazoacha athari katika shughuli za kijamii, kiuchumi, usafiri baharini na baadhi ya makazi kuzingirwa na maji.
Mikoa iliyotajwa kukumbwa na hali hiyo ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA leo Jumanne Mei 7, 2019 ambayo pia ipo kwenye tovuti ya mamlaka hiyo imeeleza kuwa wananchi wanatakiwa kujiandaa kwani kutakuwa na mawimbi, upepo mkali na mvua kubwa.
Imetaja athari hizo kuwa ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Imesema kutakuwa na kutawanyishwa/kupeperushwa kwa takataka mitaani, kuanguka kwa majani na matawi madogo ya miti, kuathirika kwa baadhi ya shughuli za uvuvi, usafiri baharini na ugumu wa upatikanaji samaki.
“Hali hiyo itakayoambatana na mvua inakadiriwa kuwapo kwa siku nne kuanzia kesho Mei 8, 2019 hadi Jumamosi ya Mei 11, 2019,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.