Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

THRDC yamuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro wa ardhi Loliondo

Mgogoro Pic Data Onesmo Olengurumwa na Afisa uchechemuzi wa Mtandao huo, Nuru Maro

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: mwananchi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutoa nafasi na kuwasikiliza wananchi wa vijiji vya Loliondo vilivyopo wilayani Ngorongoro wanaokabiliwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu.

Mgogoro huo wa muda mrefu ni kati ya wananchi na wahifadhi, Mamlaka za Hifadhi na Wizara ya Maliasili ambao unadaiwa kueendelea kukua wilayani Ngorongoro na kuleta hofu kwa jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Januari 25, 2022,  Mratibu wa Kitaifa wa THRDC,  Onesmo Olengurumwa anasema wanaamini Rais Samia akitoa nafasi ya kuwasikiliza wananchi hao huenda akawa Rais wa kwanza kupatia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya ardhi na uhifadhi wilayani Ngorongoro.

"Tunamuomba Rais Samia awape nafasi na kuwasikiliza wananchi hawa wa Loliondo ili kusikia hoja zao na hatimaye azifanyie kazi ili kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu, " amesema Olengurumwa

Olengurumwa amesema wanaiomba Serikali kusitisha mpango wake wa kuchukua ardhi za vijiji hivyo badala yake ikae na wananchi hao na kutafuta suluhu itakayokubaliwa na pande zote.

Januari 21 mwaka huu, Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela alionyesha nia ya kuchukua kilometa za mraba 1500 kutoka ardhi za vijiji vya Loliondo kwa ajili ya matumizi pekee ya uhifadhi na uwekezaji.

Olengurumwa anasema uhamisho huo wa wananchi utakapofanywa ufanywe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi na mikataba ya kimataifa.

"Tunapendekeza migogoro hii baina ya wananchi wa Ngorongoro, Loliondo na wahifadhi ufanyiwe usuluishi wa kudumu, tunapendekeza apatikane msuluhishi ambaye hana maslahi pande zote mbili au msuluhishi mkuu awe Rais Samia kwa kuwa yeye ana maslahi pande zote mbili ambapo kwa wananchi ni wapiga kura wake na wananchi wake, taasisi za Uhifadhi zipo chini yake," anasema

Chanzo: mwananchi