Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TGNP wasema Tanzania ya viwanda haitawezekana bila kumaliza ukatili wa wanawake, watoto

TGNP wasema Tanzania ya viwanda haitawezekana bila kumaliza ukatili wa wanawake, watoto

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),  Lilian Liundi amesema azma ya Tanzania ya uchumi wa viwanda haitawezekana ikiwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vitaendelea.

Ameiomba Serikali kutoa kipaumbele katika bajeti zake kuyawezesha madawati  ya jinsia, kamati za utekelezaji wa mpango kazi wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto kuanzia ngazi ya halmashauri hadi vijijini.

Amesema ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini ni janga hasa kwa nchi za Afrika, hivyo inatakiwa mikakati madhubuti na ya ubunifu.

Ameeleza hayo leo Jumatano Novemba 27, 2019 katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja vya TGNP jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yanalenga kutoa  fursa ya kutafakari na kujadili na kushirikishana mafanikio kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na kujenga mikakati na sauti ya pamoja.

“Tunashuhudia vifo vingi, ulemavu na udhalilishaji wa utu wa wanawake kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji,” amesema Liundi.

Katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya ‘kizazi cha usawa, simama dhidi ya ubakaji’,  Lilian amesema wanawake wanne kati ya 10 wanakumbana na ukatili kutoka kwa wenzi wao na hata marafiki.

Amebainisha kuwa  ripoti ya Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) ya Aprili 2019 inaonyesha kuwa wanawake 1,218 wameripoti kufanyiwa vitendo vya kikatili.

“Pia taarifa ya LHRC ya 2018 inaonyesha wastani wa watoto 394 hubakwa kila mwezi katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,  Nyanda Shuli amesema Serikali itaendelea kusimamia haki za binadamu na kuwataka wananchi kutowafumbia macho wanaojihusisha na ukatili wa wanawake na watoto.

Chanzo: mwananchi.co.tz