Shamba la miti Kawetire mkoani hapa lililoko chini Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), limesitisha shughuli za kilimo kwa wakulima wa vitongoji vya Itezi Mashariki na Machimbo Kata ya Ruiwa wilayani Mbarali baada ya kudaiwa kuingia ndani ya hifadhi.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Arnold Shoo ameliambia Mwananchi leo Jumamosi June 24, 2023 mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika Kitongoji cha Machimbo Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya. Mkutano huo ulilenga kueleza mikakati ya TFS katika kutunza hifadhi miti katika shamba hilo ikiweo kuwataka wakulima baada ya kuvuna mazao ya msimu huu kutothubutu kuzalisha tena.
“Suala lililopo ni kwa wakulima waliongia kwenye hifadhi na sio wanaolima nje ya hifadhi kwani tayari mawe ya mipaka yaliwekwa na sasa tunaanza kusafisha mipaka ili kujikinga na majanga ya moto yanayoweza kujitokeza kutokana na shughuli za kijamii,” amesema. Shoo amesema kuwa wanashangazwa na baadhi ya wakulima kukimbilia kwenye vyombo vya habari kwa madai tumewaondoa na kuwataka kubomoa makazi yao jambo ambalo sio la kweli ni uzushi wa watu wachache. “Kimsingi hilo eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 3,485 ni mali ya Serikali linalosimamiwa na TFS ambalo linapaswa kulindwa ili lije kunufaisha kizazi kijacho kuna baadhi ya wakulima wameanza kumega maeneo na kuwakodisha wenzao,” amesema. Shoo amesema kuwa endapo watalikalia kimya suala hilo kuna uwezekano mkubwa wa eneo la shamba la miti kufanyiwa uharibifu mkubwa hivyo wametoa maelekezo mara baada ya kuvuna mazao, wananchi wanapaswa kutolima tena. Kennedy Mwailamla Katibu wa Wakulima Bonde la Kawetire, Itezi Mashariki na Machimbo katika Kata ya Ruiwa, amesema kuwa wakulima hawajaridhishwa na hatua hiyo. Hivyo wameiomba Serikali kulitazama upya suala hilo. Amesema eneo hilo wananchi wameanza kuzalisha mazao na kujenga makazi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 lakini cha kushangaza leo hii Serikali inasema ni eneo la hifadhi. “Tayari TFS wanasema ni mali yao, tayari wameweka mawe, tunatakiwa kutoendeleza kwa kilimo twende wapi? Tunaomba busara zitumike kwa kuwatazama wananchi wanyonge,” amesema katibu huyo wa wakulima wa eneo hilo. Mkulima Jemsy Pilla amesema kuwa kitendo cha Serikali kuwazuia kulima kwenye maeneo ya hifadhi kitawadhoofisha kiuchumi kwani wengi wao wanategemea uchumi kwenye kilimo cha mazao mchanganyiko kwenye bonde Kawetire.