Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFS kurejesha uoto wa asili Kanda ya Ziwa

0a7f2044808db41bf589f488e83e3275 TFS kurejesha uoto wa asili Kanda ya Ziwa

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Huduma Misitu nchini (TFS), umepania kurejesha uoto wa asili uliotoweka katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti kitaifa yaliyofanyika sambamba na Siku ya Misitu Duniani, Kamishina wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, amesema kitalu maalumu cha miche ya miti ya aina mbalimbali kitaanzishwa wilayani Magu.

"Tutafanya hivyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa misitu, ili kitekeleza magizo tuliyopewa na serikali," alisema Prof. Silayo.

Maagizo hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho yaliyofanyika kwenye viwanja vya sabasaba mjini Magu leo.

Profesa Silayo alisema takwimu zinaonyesha kuwapo kwa uoto mdogo wa misitu katika mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, tofauti na maeneo mengine na kwamba hali hiyo ilianza baada ya vita kuu ya pili ya dunia.

"Miti na misitu iliyokuwapo ilikatwa na wananchi, ili kufukuza wadudu waliokuwa wakidhuru mifugo yao kama mbung'o, hadi ikaisha. Bahati mbaya hawakupanda miti mingine.

" Sasa TFS katika siku hii tunapaza sauti na kuwapa wananchi elimu juu ya umuhimu wa kurejesha uoto uliotoweka na kuendeleza uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu," alisema.

Akizungumza na wananchi, Naibu Waziri Mary Masanja, alisema Magu na wilaya nyingine za Mkoa wa Mwanza zinanyemelewa na ukame.

"Hizi ni dalili za hatari, kwani siku hizi hatupati mvua za kutosha, vyanzo vya maji vinakauka, huku kuni na miti ya kujengea sasa ni bidhaa adimu," alisema.

Masanja alitoa wito kwa wananchi kuendeleza, misitu ya uhifadhi na kuitunza na kuihudumia miti inayopandwa kote nchini.

Pamoja na kuanzishwa mara moja bustani ya kitalu cha miti, Masanja aliwaagiza TFS kuhakikisha miche ya miti mbalimbali inapatikana kwa wingi, kubaini na kuainisha maeneo sahihi ya kupanda miti na kutoa elimu ya ugani kwa wananchi waweze kutunza miti inayopandwa.

Awali, Naibu Waziri Masanja alipanda miti katika eneo la Shule ya Msingi Sagani iliyopo nje kidogo ya mji wa Magu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live