Ofisa Mtendaji wa TCCIA mkoani Arusha, Charles Makoi, alisema mpango huo wa ushirikiano, unalenga kuotesha miti 20,000 kwa mwaka huu.
“Mpaka kufikia sasa tumeshaotesha miti miti 100 katika bustani tengefu ya Mto Them (Themi Living Garden). TCCIA tumeamua kuwekeza katika masuala ya utunzaji wa mazingira ili kuihuisha zaidi sekta ya utalii na kuboresha masoko katikati ya Jiji la Arusha,”alisema
Katika taarifa yake, Makoi alisema mpango huo ulianza rasmi mwaka uliopita, kwa kupanda miti 20,000 katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame likiwemo miji ya Muriet na Morombo.
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), nayo imekuwa ikihamasisha uboreshaji wa miradi ya mazingira ya biashara na uwekezaji, kwa njia ya majadiliano ili kuwainua wananchi kiuchumi.
Naye, Ofisa Mazingira na Utalii wa Jiji la Arusha, Michael Ndaisaba, alisema mpango wa uoteshaji miti katika jiji hilo unalenga kuimarisha vivutio vya utalii katikati ya Jiji la Arusha.
Alisema mpango wa upandaji miti , ulianzia katika Kata mbalimbali za Jiji la Arusha, na kwamba hadi sasa wameotesha miti 15,000 katika kata za Muriet,Terat na Olmotony.
Ndaisaba aliwashukuru wanachama wa TCCIA, kwa kuwa wadau wakubwa wa utunzaji wa mazingira.