Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBA yasimamishwa ujenzi halmashauri

Ruvu.webp TBA yasimamishwa ujenzi halmashauri

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, ameusimamisha Wakala wa Majengo (TBA) kuendelea na ujenzi jengo la Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.

Mndeme alitangaza kuchukua uamuzi huo baada ya TBA kushindwa kukamilisha mradi huo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, licha ya serikali kutoa zaidi ya Sh. bilioni 2.2 za utekelezaji wake.

“Mimi silei wabadhirifu na wahujumu, kuanzia leo (jana) hatuwaongezei tena muda, kuanzia sasa TBA, msimame ujenzi wa jengo hili na ujenzi wake utaendelea kwa kutumia 'force account', pia ninaagiza kuanzia leo Takukuru waanze kuchunguza mradi huu," aliagiza.

Mndeme aliiagiza Takukuru kuchunguza sababu za mradi huo kusuasua na kuchukua muda mrefu na kwamba iwapo kuna mtu yeyote amefanya hujuma dhidi ya mradi huo, achukuliwe hatua haraka.

Aliwataka TBA wanapoomba kazi, kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati, akieleza kuwa licha ya kuongezewa muda wa mkataba mara mbili, bado wameshindwa kukamilisha mradi huo.

Aliwatahadharisha TBA wasihangaike kuomba kazi za ujenzi ndani ya Mkoa wa Ruvuma kwa sababu miradi yote waliokuwa wanatekeleza ndani ya Mkoa wa Ruvuma wameshindwa kuikamilisha.

Mndeme alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea, kuhakikisha anasimamia mradi huo wakati, ambao sasa unakamilishwa kwa 'force account' kwa wakati na viwango na kwamba serikali hivi sasa inatekeleza kwa wakati na viwango miradi mingi kwa 'force account'.

Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka Kampuni ya BICO, Ahmed Nyange, alisema mradi huo ambao umefikia asilimia 84, ulitarajiwa kukamilika Januari 20 mwaka huu, lakini mkandarasi aliongezwa miezi minne hadi Mei 31 mwaka na ameshinda kukamilisha mradi.

Nyange alisema hadi sasa mkandarasi ameshalipwa zaidi ya Sh. bilioni moja, sawa na asilimia 61 ya gharama yote ya mradi na kwamba mkandarasi ameshindwa kukamilisha mradi kwa wakati, hivyo BICO inaunga mkono kukamilisha mradi kwa 'force account'.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Shafii Mpenda, alisema TBA imekuwa na dosari nyingi ambazo zimekuwa zinajitokeza mara kwa mara na kusababisha mradi kushindwa kukamilika kwa wakati.

“Ninasikitika kusema kwamba imebidi tufikie hapa tulipofika ili kunusuru mradi na fedha za umma, tusitishe mkataba na TBA na tuombe ridhaa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Tamisemi, ili aridhie kukamilisha kazi zilizobaki kwa kutumia 'force account'," alisema.

Awali, Mwakilishi wa TBA, Elias Tillya, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuwa walianza vizuri utekelezaji wa mradi huo na walitarajia Juni mwaka huu kukabidhi jengo hilo.

Hata hivyo, alisema kuwa mwishoni mwa Mei mwaka huu, TBA ilipata vikwazo kwenye akaunti zake katika mikoa yote nchini, hali ambayo ilisababisha kushindwa kutoa fedha baada ya akaunti zake zote kuzuiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live