Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetekeleza kwa vitendo agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kupunguza bei za nyumba za Magomeni Kota baada ya awali wakazi hao kugomea mkataba ulioletwa.
Machi 23, 2021, Rais Samia wakati akizindua nyumba hizo aliitaka TBA kupunguza gharama za uuzaji wa nyumba hizo kwani zipo juu kwa wananchi wa kawaida
Awali, nyumba hizo zilikuwa zikiuzwa kwa Sh74 milioni kwa chumba na sebule na Sh86 milioni kwa vyumba viwili na sebule.
Februari 6, 2023, wakazi 644 wa Magomeni Kota waligomea kusaini mkataba wa kuanza kununua nyumba hizo kwa madai kwamba bei waliyoletewa sio rafiki na haiendani na hali zao za kiuchumi.
Hayo yameelezwa leo Februari 14, 2023, jijini hapa na Mtendaji Mkuu wa TBA, Daudi Kandoro wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wakala huo kwa mwaka 2022 – 2023.
Mtendaji huyo amesema baada ya maagizo ya Rais walikutana na timu ya watalaamu na kujadiliana namna ya kunguza bei ya nyumba hizo.
Amesema nyumba ya chumba kimoja imepunguzwa kutoka Sh74.8 milioni na sasa itauzwa Sh48 milioni na ile ya nyumba viwili imepunguzwa kutoka Sh86 milioni hadi Sh56.9 milioni.
Amesema kutokana na maelekezo ya Rais Samia, wameweza kupunguza Sh18.2 bilioni.
Mtendaji huyo amesema wamepunguza bei ya nyumba hizo mara baada ya kuondoa gharama za ardhi, maeneo jumuishi kama korido, mandhari ya nje, mashimo ya maji taka na vizimba vya taka ngumu vilivyokuwa vimejumuishwa awali.
“Timu imekubaliana deni litarudishwa kwa miaka 15 na miaka mitano watakaa bure lakini hakutakuwa na riba. Niseme hakuna sakata kwa upande wa wakala tunatambua umoja wa wanakota,” amesema mtendaji huyo.
Kuhusu madai ya miradi kujengwa chini ya kiwango, Kondoro amesema jambo hilo sio la kweli na TBA ina wataalamu wa kutosha ambao wamekuwa wakitumia weledi katika kazi zao.
Amezungumzia maneno yaliyojitokeza wakati wa mradi wa hosteli za Magufuli kutokuwa na ubora akisema yaliyojitokeza wakati ule yalikuwa ni bahati mbaya kutokana na kutokufungwa kwa eneo ambalo kitaalamu linaitwa “Expension Joint”.
“Bado tuna changamoto ya watumishi, mahitaji ni 811 lakini waliopo ni 350. Tunashukuru Serikali imetupa kibali na tutaanza kuajiri. Bado tuna changamoto ya vifaa ikiwemo upatikanaji wa kokoto,” amesema mtendaji huyo.