Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TARURA yabaini mchezo ada za maegesho Dar

Maegesho TARURA yabaini mchezo ada za maegesho Dar

Fri, 31 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) jijini hapa umeshtukia mchezo mchafu unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wakusanya ushuru wanaotoa huduma katika maegesho na baadhi ya wateja wanaotumia huduma hizo.

Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga alisema hayo, alipozungumza na Mwananchi lililotaka kujua mwenendo wa mfumo wa ulipaji wa ada za maegesho ya magari, awamu ya pili iliyoanza Desemba mosi, mwaka huu.

Mwananchi ilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa huduma hiyo wakidai kubambikiwa madeni.

Mkinga alisema wakusanya ushuru hao hufanya mazungumzo haramu na wateja wao kulipana fedha nje ya mfumo ambazo hazifiki ofisini.

Alikiri kuwa baadhi ya wenye magari hubambikiwa madeni hayo baada ya wakusanya ushuru kuyapiga picha magari na kuyaingiza kwenye mfumo kuwa wanadaiwa, wakati hata hawakuyaegesha kwenye maegesho ya Tarura.

Hata hivyo, alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka waonyeshe wamefanya kazi wakati wanawaumiza baadhi ya wateja ambao hawakustahili na kuwaacha wale wanaofanya nao mazungumzo ya pembeni.

“Wanamwambia mteja tupe buku (Sh1,000) ili asiipige picha gari yake kwa ajili ya kuiangalia na kuingiza katika mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao. Kufanya hivi ni kuikosesha mapato Serikali na kuwaingiza kwenye madeni wale wasiostahili, tumeshaijua hii mbinu baada ya kupata taarifa kutoka kwa wateja wema,” alisema Mkinga.

“Tukishirikiana na mzabuni, tayari tumewaondoa baadhi yao katika vituo vyao vya kazi kwenye maeneo ya Posta uelekeo wa Feri-Kigamboni, Kariakoo, Millenium Tower na Lumumba.Tunafahamu baadhi ya mawakala hawaupendi mfumo huu kwa sababu hawapigi fedha.”

Alisema Tarura imebaini pia kuwapo kwa vitendo hivyo, alivyovifananisha na uhalifu, baada ya kupata taarifa zenye ushahidi kwa nyakati tofauti kutoka kwa wasamaria wema. Mkinga aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tarura ili kuvikomesha vitendo hivyo.

“Tunaomba wananchi wasikubali vitendo au makubaliano yaliyo kinyume na utaratibu kati yao na wakusanya ushuru hao kuhusu ulipaji wa ada za maegesho,” alisema Mkinga.

Ili kulitatua hilo, Mkinga alisema Tarura imeunda mkakati wa timu ya wataalamu inayofanya tathmini na usimamizi kwa kupita katika maegesho yao yote ili kubaini vyombo vya moto ambavyo havijaingizwa kwenye mfumo wa ulipaji.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala ya Asceric Limited inayofanya kazi ya kukusanya ushuru wa ada za maegesho ya Tarura, Mathayo Nungu alisema, “ni kweli kuna vitendo hivi na tuna wafanyakazi zaidi ya 400 ndiyo maana kuna hii changamoto, si wote wanaweza kuwa waaminifu.”

Alisema tayari wameshawafukuza kazi zaidi ya wakusanya ushuru 10 baada ya kuthibitika kukiuka utaratibu wa kazi.

Akizungumzia mwenendo wa mfumo huo tangu Desemba mosi, Mkinga alisema baadhi ya wananchi wameanza kuuelewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live