Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TARURA Same kutumia Sh3 bilioni matengenezo ya barabara

Pesa Fedhaddd TARURA Same kutumia Sh3 bilioni matengenezo ya barabara

Wed, 2 Feb 2022 Chanzo: mwananchidigital

Kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, kimepitisha bajeti ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ya Sh3 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya barabara mbalimbali za wilaya hiyo.

Wilaya ya Same yenye majimbo ya Same Mashariki na Same Magharibi, ina mtandao mkubwa wa barabara za vijijini ambapo hadi kufikia mwaka wa fedha 2022/2023, kilometa 870 zimesajiliwa na Tarura katika wilaya hiyo.

Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi 6 ya barabara katika Jimbo la Same Magharibi linaloongozwa na Mbunge Dk Mathayo David na miradi 6 kwa upande wa Same Mashariki linaloongozwa na Mbunge wake, Anne Kilango Malecela.

Akizungumza leo Februari 02, 2022 kwenye kikao hicho, Meneja wa Tarura Wilaya ya Same, Mhandisi Mnene Nyamega amesema bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya mara nne kwa kuwa miaka ya nyuma walikuwa wakipokea bajeti ya Sh700 milioni.

"Kweli tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita ambayo imefanya mapinduzi makubwa ya maendeleo ya barabara Nchini maana haijawahi kutokea kupata bajeti kubwa namna hii tokea Tarura imeanza mwaka 2017,"amesema.

Amesema kutokana na Jiografia ya maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo kuwa milimani na barabara zake kuwa na mwinuko mkali na kuleta changamoto ya usafiri kwa wananchi, bajeti hiyo inakwenda kufungua mawasiliano zaidi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapende amesema changamoto kubwa kwa barabara za vijijini ni utelezi wakati wa mvua hivyo kuhimiza Tarura kutengeneza barabara hizo kwa kiwango bora cha changarawe.

Pia alipendekeza baadhi ya barabara zitengenezwe kwa zege kwa yale maeneo korofi zaidi, mapendekezo ambayo Meneja wa Tarura aliyafiki akisema ni kati ya mpango kazi wake aliojiwekea ili kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote.

Madiwani Casim Mnyone wa Kata ya Bangalala, Mshinwa Banzi wa Kata ya Suji na Gaitani Mkwizu Kata ya Mshewa wameupongeza uongozi wa Tarura Wilayani hapo kwa mipango hiyo wakiomba washirikiane nao kubaini maeneo korofi.

Chanzo: mwananchidigital