Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TARI Uyole wasambaza teknolojia ya kilimo hifadhi

80b1cecef9a77d6638369916c105c915 TARI Uyole wasambaza teknolojia ya kilimo hifadhi

Sat, 28 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Uyole mkoani Mbeya, inaendelea kusambaza teknolojia ya kilimo hifadhi kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji.

Mkurugenzi wa TARI Uyole, Dk Tulole Bucheyeki alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO kuhusu teknolojia hiyo ya kilimo hifadhi baada ya kukagua majaribio yake.

Dk Bucheyeki alisema kituo hicho kimekuwa kikisambaza teknolojia hiyo kwa wananchi kwa kuwa imefanyiwa utafiti na kuonekana kuwa ina manufaa makubwa katika kilimo kwa kuwa haina gharama kubwa.

Kuhusu teknolojia hiyo ya kilimo hifadhi, Mratibu wa Utafiti katika kituo hicho cha Uyole, Dk Ndabhemeye Mlengera alisema kilimo hicho kina kanuni tatu, ikiwemo kutosumbua udongo kwa kiasi kikubwa, kufunika ardhi wakati wote kwa mazao funika au masalia ya mazao ikiwa ni pamoja na mzunguko wa mazao aina ya nafaka na mikunde.

Alisema kilimo hicho kina faida kubwa itokanayo na uvunaji maji kwa njia ya kuchora mifereji, hivyo kusaidia mazao kuendelea kukua hata kama mvua itakuwa ni chache na kuongeza tija.

Kwa upande wake Mtafiti wa Kilimo hicho, Adolph Katunzi alisema tafiti za kilimo hifadhi zimefanywa katika mazao ya mahindi, maharage, ngano, mpunga na soya.

“Kwa upande wa zao la maharage, mbegu zilizopandwa kwa kutumia teknolojia ya Kilimo hifadhi ni Uyole 96, Njano Uyole na Calima Uyole. Mbegu zote ni nzuri na hulimwa kulingana na uhitaji wa soko kwa mlaji.

“Kwa mfano, Njano Uyole ni mbegu inayopendwa hasa katika mahoteli na nchi jirani kama Rwanda kutokana na ladha yake kwa walaji. Pia kwa upande wa soko, mbegu ya Njano Uyole pamoja na Uyole 96 huuzwa kwa bei ya elfu 50 kwa debe,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo alisema ili kuinua zaidi uchumi wa kati na wa wakulima, Tanzania inapaswa kutumia teknolojia mbalimbali zinazotoa majibu chanya kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi katika taasisi hiyo, Dk Yohana Budeba alisema kilimo ni uti wa mgongo nchini, hivyo anaipongeza serikali kwa kuanzisha TARI kwa kuwa imeleta mageuzi ya kilimo nchini kwa kujibu changamoto za wakulima kupitia utafiti unaofanywa.

Chanzo: habarileo.co.tz