Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu aibua tatizo la vyoo shuleni

Sat, 5 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema licha ya nguvu nyingi za wadau na Serikali kuelekeza kwenye ujenzi na ukarabati wa madawati na madarasa, lakini kuna tatizo kubwa la shule nyingi za msingi jijini hapa kukosa vyoo jambo linalohatarisha usalama wa wanafunzi.

Sugu alisema hayo jana wakati akizungumza na wazazi na wananchi wa Mabatini jijini hapa alipokuwa anakabidhi vifaa vya ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Mabatini vilivyogharimu Sh4 milioni.

Alisema kutokana na hali hiyo, ameamua kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo kuendesha kampeni ya kuboresha vyoo kwa shule zote zenye uhitaji na ametoa zaidi ya Sh30 milioni kwa shule sita za msingi na moja ya sekondari kwa ajili ya ujenzi huo akiwa na kauli mbiu ya ‘Vyoo kwanza shuleni’.

“Baada ya kuona kwenye madarasa na madawati tunaenda vizuri, nimeamua kuwekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa vyoo kwa kushirikiana na wazazi,” alisema.

Diwani wa Kata ya Mabatini, Lazaro Ngonyani alisema wamepokea Sh4 milioni na wamefanya manunuzi ya mbao, misumari, saruji, bati na kuwalipa mafundi lakini pia wananchi wamechangia matofali na ujenzi hadi kwenye lenta.

Ofisa Mtendaji wa kata ya Kalobe, Felix Charles alisema wamepokea Sh5 milioni za ujenzi wa vyoo Shule ya Msingi Kalobe.



Chanzo: mwananchi.co.tz