Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sua, Pass kuwezesha wahitimu ujasiriamali

Mon, 23 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Taasisi binafsi ya kusaidia sekta ya kilimo Tanzania (Pass) imetenga Sh2 bilioni kwa ajili kuwawezesha wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) kuanzisha miradi ya kilimo na biashara. 

Upatikanaji wa fedha hizo umelenga uanzishwaji wa miradi 100 ya majaribio katika chuo hicho kupitia mpango maalumu wa utoaji kazi na majaribio kupitia vituo maalumu vya kutoa uzoefu kwa wajasiriamali vijana. 

Hayo yamesemwa leo Julai 23, 2018 na mkurugenzi mtendaji wa Pass, Nicomed Bohay baada ya kutiliana saini makubaliano na Sua ya kuwaandaa kwa vitendo wajasiriamali vijana ambao ni wahitimu wa fani mbalimbali wa chuo hicho. 

“Baada ya kuona uwapo wa changamoto ya ajira kwa wahitimu wa fani za kilimo na wengine kushindwa kujiajiri kwenye kilimo kutokana na kukosa mitaji, Pass kupitia idara yake ya kilimo biashara na ubunifu iliamua ije na mpango huu,” amesema Bohay. 

Amesema mpango huo utawezesha wajasiriamali vijana kupata mitaji pamoja na vyenzo mbalimbali katika maeneo maalumu kwa lengo kuwaandaa kuwa wajasiriamali watakaoweza kumiliki miradi ya kilimo biashara. 

Naye makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Raphael Chibuda amesema ushirikiano wao na Pass umekuja wakati mwafaka na kuwataka wahitimu na watafiti wa chuo hicho kuchangamkia fursa hiyo. 

Prrofesa Chibuda amesema chuo hicho kimetoa eneo la kutosheleza miradi ya wajasiriamali vijana kwa lengo la kuhakikisha vijana wanajiajiri kuondokana na changamoto ya kutembea na wasifu kutafuta ajira. 

 Mwenyekiti wa bodi ya chama cha wajasiriamali wahitimu wa Sua Sugeco, Dk Anna Temu amesema makubaliano hayo ya Pass na Sua yatasaidia kutekeleza lengo la kuwa na nchi ya uchumi wa viwanda.

Dk Temu amesema Sugeco imesaidia uanzishwaji wa kampuni mbalimbali za uzalishaji  kupitia sekta ya kilimo, hivyo makubaliano hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wajasiriamali na kampuni. 

Chanzo: mwananchi.co.tz