Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stendi Njombe yajengwa usiku, Takukuru yasaka waliofilisi benki

54756 Pic+stend

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/ Songea. Zikiwa zimesalia siku 10 tangu Rais John Magufuli kutoa siku 30 kwa uongozi wa mkoa wa Njombe na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha ujenzi wa stendi ya Njombe unakamilika, sasa unafanyika usiku na mchana.

Pia, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Ruvuma imeanza uchunguzi wa kufuatilia waliofilisi Benki ya Wananchi Mbinga (MCB).

Aprili 10, akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, Rais Magufuli alitoa agizo hilo kufuatia ujenzi wa muda mrefu huku akitaka uchunguzi kubaini upungufu na wahusika wachukuliwe hatua.

Jana, mkuu wa mkoa huo, Christopher ole Sendeka alilieleza Mwananchi lililotaka kujua utekelezaji ulipofikia kuwa maagizo ya Rais yanatekelezwa na tayari kazi inafanywa kwa kiwango cha juu.

Rais Magufuli aliutaka uongozi wa mkoa huo kuhakikisha ndani ya siku 20 stendi hiyo inakamilika.

Kuhusu uchunguzi wa benki ya Mbinga ambao Rais Magufuli aliagiza ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua, kamanda wa Takukuru mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka, alisema tayari wameanza kufanya uchunguzi.

Chagaka alisema tayari wameomba nyaraka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuwasaidia kufuatilia.

“Tumeanza kufanya uchunguzi wa awali kwa kuwasiliana na Benki Kuu na tumewaomba watusaidie nyaraka mbalimbali ambazo zitatusaidia kufanya ufuatiliaji, hivyo tunasubiri ili tuendelee na hatua inayofuata kwani ndiyo wanaojua benki ilifilisikaje hadi wakaifunga,” alisema Chagaka.

Aprili 7, Rais Magufuli akiwa wilayani Mbinga alitoa agizo kwa vyombo vya dola kumpata aliyefilisi benki hiyo ili kukata mzizi wa fitina. Agizo hilo alilitoa kufuatia Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda, kumuomba amsaidie kuvichukulia hatua vyama vya ushirika vilivyoibia wakulima kahawa.



Chanzo: mwananchi.co.tz