Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stella Jairosi: Uzalishaji wa viongozi walemavu ni vita endelevu nchini

45075 Stella+pic Stella Jairosi: Uzalishaji wa viongozi walemavu ni vita endelevu nchini

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tafiti na ushahidi wa matukio mbalimbali bado yanaonyesha kuzaliwa mtoto wa kike katika jamii ya Kitanzania bado ni changamoto. Lakini, mtoto wa kike anapokuwa mlemavu vikwazo huongezeka zaidi katika jamii inayojiendesha kwa mfumo dume na mila potofu nchini.

Wapo wanaofungiwa ndani, kutupwa, kuuawa au kufanyiwa ukatili wa kila aina hatua inayowafanya kujiona wao siyo sawa na kizazi kingine duniani. Hatua hii inaua vipaji vingi vya uongozi katika kundi la walemavu hao.

Kutokana na changamoto hiyo, Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (Swauta), ikaamua kuanzisha vita ya kupambana na hali hiyo. Hili ni kundi la wanachama zaidi ya 600 nchini walemavu wanaoendesha shughuli mbalimbali za kuibua na kusaidia mwanamke mlemavu ili kujikomboa.

Mwaka 2014, Swauta iliendesha programu ya kutafuta viongozi walemavu walioshiriki kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015, kazi iliyofanikiwa baada ya kupata madiwani sita (Watano CCM na mmoja Chadema).

Viongozi hao walipatikana kutoka kundi la walemavu zaidi ya 200 waliofanyiwa mafunzo katika mikoa mbalimbali kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na mwanamke, ‘UN Women’ na mwaka huu wamejipanga lakini mitihani bado ni mingi katika jamii.

Katika mahojiano na gazeti hili, mwenyekiti wa kikundi hicho, Stella Jairosi anasema tayari walishafahamu changamoto zilizoonekana kuwa kikwazo kwa mwaka 2014.

Mwandishi: Changamoto gani mlizogundua na mnafanya nini ili kuwafikia wengi na washiriki kutimiza ndoto zao za uongozi?

Stella: Tuligundua kwamba, walemavu wengi vijijini na mikoani hawana ujasiri kabisa licha ya kuonekana kuwa na vipaji vya kuongoza. Lakini tatizo tulichelewa kuanza kazi ya uhamasishaji na utoaji wa elimu 2014, wakati huo wanasiasa wenzao walikuwa wameshajipanga mwaka mzima kujinadi.

This time (safari hii) tumeweza kupata ufadhili wa shirika jingine la Hanns Seidel Foundation, ambao hutoa mafunzo ya uongozi kwa mwanamke, sasa wamechukua wanachama wetu watatu kuwaandaa katika programu yao ya mwaka mmoja na nusu, itakayomalizika Mei mwaka huu.

Pia, tulipeleka wanachama wanne katika programu ya mwaka mmoja iliyoendeshwa na Shirika la Kijerumani la SES, linalofanya mafunzo ya uongozi kila mwaka. Walishamaliza mwaka jana Novemba hao.

Hatua yote hii ni kujiandaa kwa ajili ya kuwapata wanachama watakaokuwa wamepata mbinu mbalimbali uongozi na tutawapeleka maeneo ya vijijini ili kuwafundisha wanawake walemavu wanaotaka kugombea.

Mwandishi: Hapa nchini kuna mashirika mengi yanatoa mafunzo ya uongozi, Swauta inatumia vipi nafasi hiyo kuunganisha wanachama wake ili kupata wakufunzi wengi zaidi nchini?

Stella: Mwanzoni mafunzo haya yaliendeshwa bila kuhusisha wenye ulemavu, wakilalamikia changamoto ya kuwafundisha walemavu wanaotaka kugombea nafasi za uongozi.

Pamoja na vikwazo hivyo, tulifanikiwa kupata viongozi wazuri tu na mmoja aliwahi kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Ukerewe ni mlemavu, jina limenitoka kidogo. Katika nafasi ya wabunge, tulipata watatu na mmoja alifariki mwaka juzi, Dk Elly Macha wa Chadema. Nafasi za wenyeviti wa serikali mitaa na kuna baadhi walipata katika Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake (UWT), huko Arusha.

Mimi niliwahi kufanya kazi katika Idara ya Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu makao makuu nikiwa mwalimu kitaaluma na kwa sasa niko Taasisi ya Elimu nchini, katika uhakiki wa vitabu vya kitaaluma tangu Julai mwaka jana.

Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba, tumeanzisha Swauta mwaka 2007, tumeshafika mikoa minne, tumeshuhudia vikwazo kwa miaka zaidi ya 10 kwa mwanamke tena mwenye ulemavu ila matumaini ni makubwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz