Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sonjo, kabila lililo Ngorongoro lenye lafudhi sawa na Wakurya

Dc9e99f9ad6e35e750dc89405603e1f8.png Sonjo, kabila lililo Ngorongoro lenye lafudhi sawa na Wakurya

Fri, 24 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SONJO ni kabila dogo la kibantu, linalopatikana kaskazini mwa Tanzania, kilometa 100 kutoka magharibi mwa ziwa Natron katika wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Manyara.

Wataalamu wa masuala ya lugha wanasema sauti na lafudhi ya lugha ya Wasonjo, inashabihiana na lugha ya Wakuria lililopo Mashariki mwa ziwa Victoria katika mkoa wa Mara. Hata hivyo, muundo wa maneno baina ya lugha hizo mbili unatofautiana.

Pia simulizi za kale zinaeleza kuwa ingawa kabila la Wasonjo lina uhusiano na kabila la Wakurya kwa kuwa chimbuko la makabila hayo liko Serengeti, lakini lugha na utamaduni wa makabila hayo haufanani.

Kama yalivyo makabila mengine, Wasonjo wanajishughulisha na kilimo na ufugaji. Kabila hilo linalima mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na mahindi, viazi, maharage. Pia hujishughulisha na ufugaji wa mbuzi, ng’ombe na nyuki. Kila familia ilitundika mizinga katika miti kwa ajili ya kuzalisha asali. Miti iliyomilikiwa na viongozi wa jadi ilibeba mizinga ya familia tofauti.

Asali iliyopatikana ilitumika kama sehemu ya mlo wa chakula pia kutengeneza pombe ya asili inayojulikana kama Bukhoma. Sifa ya kipekee kwa kabila hilo ni kuishi katikati ya jamii ya wafugaji wa Kimasai, jambo linalosababisha baadhi ya watu kudhani kuwa kabila hilo ni jamii ya lugha ya Nailoti kama ilivyo kwa Wamasai. Kabila hilo limejitenga na makabila mengine ya kibantu na mfumo wao wa maisha ni tofauti ikilinganishwa na mfumo wa makabila mengine ya kibantu.

Hata hivyo, watafiti mbalimbali wa mila na tamaduni za makabila wanathibitisha kuwa Wasonjo ni Wabantu ingawa baadhi ya tamaduni zao zinafanana na zile za kabila la Kimasai.

Historia ya makabila kwa njia ya simulizi inaonesha kwamba jina halisi la kabila la Wasonjo ni Batemi ila wakoloni waliovamia kanda ya Afrika Mashariki ndio waliwabatiza jina la Wasonjo.

Inasemekana kuwa wakati wakoloni wa Kiingereza walipofika katika eneo la Wasonjo waliwakuta wakivuna kunde zilizojulikana kwa jina la Sonjo. Wageni hao walibaini kuwa wenyeji wao walikuwa na umakini mkubwa katika kukizingatia majira ya kilimo.

Kwa kuwa shughuli ya uvunaji ilikuwa ya kipekee wageni walibaini kuwa kila wanapopita wanakutana na kunde hizo maarufu kwa jina la Sonjo ndipo wakaanza kustaajabu na kusema kila sehemu ni “sonjo… na nchi hii imekuwa ya Sonjo.”

Kutokana na ukaribu wa Kiafrika, wazee walikubali ardhi yao kubatizwa jina la Sonjo na jina likaenea na kupata umaarufu kiasi cha kusababisha kabila hilo kujulikana kama Sonjo badala ya Batemi.

Mwandishi wa kitabu cha hivi karibuni kuhusu makabila ya kaskazini mashariki mwa Tanzania, Gervase Mlola, anasema kuwa ingawa kabila hilo ni maarufu kama Wasonjo, wenywe wanajiita Wabatemi.

Mlola anafahamisha kuwa Wasonjo wanapenda kujiita Wabatemi ili kuhifadhi kumbukumbu ya asili yao. Inasemekana kuwa awali kabila hilo lilikuwa linaishi eneo lililojulikana kama Batemi. Walilazimika kuhama makazi yao ya asili baada ya kukumbwa na baa la njaa hivyo kuhamia eneo walipo sasa ambapo lina ardhi inayofaa kwa kilimo na maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Kwa mujibu wa simulizi za kale Wasonjo walipokabiliwa na baa la njaa mzee maarufu kwa jina Mwegumune alipewa maono kwamba wanapaswa kuhama eneo la Batemi na kwenda eneo walilopo sasa kwa kuwa lina maji ya kutosha kuendeleza kilimo na ufugaji. Kama ilivyo kwa makabila mengine, Wasonjo walikuwa na dini ya asili ya Afrika na Mungu wao alijulikana kama Hembague.

Mtafiti anayefahamika kwa jina moja la Fosbrooke anasema kuwa imani ya kabila hilo inashabihiana na imani ya Kristo kwa kuwa waliamini kuwa Hambague aliyeondoka duniani atarejea tena siku za mwisho.

Hembague alikuwa mtabiri, mshauri na anawatia moyo watu. Fosbrooke amewanukuu Wasonjo wakisema kuwa Mungu wao hakuzaliwa wala hana wazazi bali alishuka kutoka mawinguni na mwisho wa siku atarudi akitokea huko. Watu hawa pia wana itikadi kali, imani na masharti magumu sana katika suala la dini ambapo hata kwa makabila mengine Afrika hushindwa kupenda, kuiga au hata kujifunza.

Viongozi wa dini hiyo hupatikana kwa urithishanaji kwa kuzingatia vyeo mbalimbali kama makuhani, manabii na mapadri kutoka ngazi ya chini hadi juu. Dini ya Sonjo huhusisha tamaduni za dini zilizopo duniani kote ikiwemo dini ya Kikristo ambayo mambo mengi yalifanana na ya dini ya watu wa Sonjo ikiwemo kubatiza kwa kutumia maji.

Lakini pia katika suala la dini watu wa Sonjo waliheshimu sana mavazi yao maalumu ya jadi kwa ajili ya kwenda katika sala. Fosbrooke aliwanukuu Wasonjo wakisema, “kwa sasa Hembague yuko katika safari na atarudi Sonjo siku za mwisho wa dunia.

Wasonjo wanaamini kuwa siku ya kurudi kwa Mungu wao jua litatokea magharibi na mashariki kisha litakutana katikati na kusababisha moto, moshi mzito na kelele za ajabu. Tukio hilo litakapotokea ndege wote wataruka kwenda msituni na hapo Hembague atatokea kwa ajili ya kutafuta wanaume wote watakaokuwa na alama za kipekee katika titi na bega la kushoto.

Kutokana na imani hiyo, Wasonjo wanavaa mavazi ya asili yanayofana na ya Kimasai na unaweza kuwatofautisha kwa kuangalia kimo na ufungaji wa vazi husika. Wanawake na wanaume wa Kisonjo hutoboa masikio na kuvaa hereni mithili ya Masai ila wana alama ya kipekee katika titi na bega la kushoto ili watu na Mungu wao aweze kuwatambua kwa urahisi.

Sonjo na Wamasai walikutana na kuishi kama marafiki na hicho kinaweza kuwa kielelezo kipekee cha historia yao. Hata uhusiano wao ulivunjika baada ya kila kabila kuwa kubwa na kutaka kuwa na wigo mpana zaidi wa maeneo ya malisho hivyo migogoro ya mipaka kati ya pande hizi mbili ulizuka. Hata watafiti wa makabila na tamaduni wanaamini kuna mambo mengi yanafanana sana katika makabila hayo mawili.

Pia utafiti wa hivi karibuni unasema unasema Sonjo inawezekana walitokana na kabila la Segeju lililopo Tanga kwa sababu jamii hiyo walijenga makazi yao kama ya watu wa Segeju. Sifa nyingine kuu kwa kabila hilo ni mfumo wao wa asili kwa kilimo cha umwagiliaji. Mfumo huo umesababisha baadhi ya wataalamu kuhisi kuwa Wasonjo wanatokana na watu wa kale wa kabila la Engaruka ambalo lilipotea. Hata hivyo, utafiti wa kina aliofanya John Sutton unabainisha kuwa Wasonjo hawana utaalamu wa kutumia mawe kuzuia mmomonyoko wa udongo kama ilivyokuwa kwa kabila la Engaruka. Vilevile kilimo cha umwagiliaji kwa Wasonjo kimewatambulisha kimataifa kwani hata wataalamu wanaosoma na kufanya tafiti za maendeleo katika jamii za kale hupenda kutumia kabila la Sonjo kwa kupata takwimu nzuri na sahihi zaidi. Watu wa himaya ya Sonjo waliishi kama ndugu katika familia zenye watu sita sita zilizozungushiwa uzio. Kila familia ilikuwa na eneo maalumu. Pia wana eneo maalumu maarufu kwa jina la Keritone ambalo hutumika kwa ajili ya mikutano na mitambiko pia kwa sherehe mbalimbali ikiwa ni pamoja na shukrani kwa ajili ya mavuno. Sherehe maarufu ilijulikana kama Mbarimbari na huadhimishwa mara moja kila mwaka kama shukrani kwa Mungu kwa kuwalinda na kuwapatia baraka. Hata hivyo, Wasonjo hawajaachwa nyuma kimaendeleo kwa kuwa baadhi yao wameondokana na mila na desturi za kiafrika na wanafuata dini mbalimbali zilizoletwa na wageni. Pia Wasonjo wameboresha kilimo kwa kuzingatia mfumo wa kisasa. Wameacha mfumo wao wa zamani na hivi sasa wametawanyika ili kupanua maeneo ya kilimo cha umwagiliaji pia kwa ajili ya kuweka huduma za kijamii kama shule, zahanati na masoko. Kwa mujibu wa mila na desturi za Wasonjo, ndoa inahusisha mke na mume mmoja. Kaya moja huwa na watu wengi tegemezi na kila familia iliona ufahari kujumuisha watoto wa kike na wa kiume, babu, bibi, mjomba, baba mdogo, shangazi, binamu ndugu na jamaa.

Chanzo: habarileo.co.tz