Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Songwe kuwasaka watoto 1,000 waliokimbia shule

WANAFUNZI NUSU Songwe kuwasaka watoto 1,000 waliokimbia shule

Sat, 23 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mkuu wa wilaya ya Songwe, Simon Simalenga amesema wamejipanga kuanzisha oparesheni ya kuwasaka watoto zaidi ya 1,000 ambao hawafiki shuleni ili kukomesha tatizo la utoro kwenye shule za msingi zilizopo katika halmashauri ya Songwe mkoani Songwe.

Simalenga ametoa kauli hiyo Oktoba 21 kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza katika mwaka wa fedha 2021/22

Amesema atahakikisha wazazi wa watoto hao wanasakwa ili waweze kuwahamasisha watoto wao kuendelea na masomo.

“Siwezi kukubali watoto zaidi ya 1,000 kutofika shule lazima wazazi wa watoto hawa wafuatiliwe ambapo amesema atahakikisha watoto wote wanaozurura wanakamatwa na kurudishwa shuleni,” alisema Simalenga.

Simalenga amewaomba madiwani wa halmshauri hiyo kuhakikisha wanakaa na wazazi na kuwaeleza umuhimu wa elimu ili kukomesha suala la utoro na kujenga taifa lililo salama kwamadai mtoto anapokuwa mtaani hujiingiza kwenye makundi hatarishi.

Ofisa elimu wa shule za msingi katika halmashauri ya Songwe, Michael Nzunda amesema tatizo la utoro sugu kwenye shule za msingi zilizopo katika halmshauri hiyo umetajwa kuwa ni moja ya changamoto inayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo na kwamba wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti hali hiyo.

Nzunda amesema tayari wamewarejesha shuleni watoto 200 na kwamba wanaendelea kuwafuatilia watoto 1,000 ili waweze kuendelea na masomo.

Ofisa huyo alibainisha sababu tano zinazochangia tatizo la utoro katika halmashauri hiyo kuwa ni shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu, ufugaji, uvuvi, umbali wa shule ambapo amesema baadhi ya watoto hutembea umbali wa zaidi ya kilometa 15 kufuta shule.

Philipo Mulugo ambaye ni mbunge wa jimbo la Songwe, alisema amesikitishwa na idadi hiyo ya wanafunzi hao kutofika Shule ambapo amesema atahakikisha anaungana na mkuu wa wilaya katika kukomesha tatizo hilo la utoro kwa halmashauri ya Songwe.

Chanzo: mwananchidigital