Mlipuko unaodhaniwa kusababishwa na baruti umetokea jana Jumanne, Aprili 13, 2021 katika Kata ya Saza Wilaya ya Songwe na kusababisha madhara kwenye baadhi ya nyumba za wakazi wa maeneo ya karibu na tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samweli Opulukwa amesema mlipuko huo umeanzia katika majengo yanayotumika kuhifadhi baruti ambapo kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo inachunguza ikiwa ni pamoja na kubaini kama kuna watu waliopata madhara.
“Serikali inatoa onyo kwa wachimbaji wanaotumia baruti kuwajibika kuzitunza ili zisilete maafa,” amesema Opulukwa.
Aidha, Mwenyekiti wa mtaa wa Saza, Philpo Patrick amesema mlipuko huo umeleta taharuki kwa wakazi wa eneo hilo na kuwa umetokea katika majengo yanayohifadhi baruti.