Kampuni ya Kimataifa ya Refocus Africa yenye Makao Makuu yake Texas, Marekani na ambayo inaundwa na Wazawa kutoka Nchi mbalimbali Africa wanaoishi Marekani, kupitia mradi wao wa ‘Smart City Technology’ yaani ujenzi wa Mji unaotumia teknolojia ya kisasa wametangaza rasmi nia ya kwenda kuwekeza Pangani Mkoani Tanga hii ikiwa ni sehemu ya matokeo chanya ya Royal Tour ya Rais Dkt. Samia aliyoizindua Marekani.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka kwa Wawekezaji hao Jijini Dar es salaam, amesema Mradi huu ambao utekelezaji wake utachukua miaka mitano upo kwenye hatua za awali za utekelezaji na utagharimu zaidi ya USD Bilioni 1 na utawekezwa kwenye Ekari Elfu moja kwenye eneo la kilimo, viwanda na mitambo ya usindikaji, ujenzi wa nyumba pamoja na Hotel za kisasa na vituo vya kisasa vya burudani, ujenzi wa viwanja vya kisasa vya michezo, shule za kisasa, kumbi, ofisi na shopping malls za kisasa.
Wanufaika wakubwa wa mradi huu ni wazawa maana watapatiwa elimu, ajira na ujuzi wa kutosha kwenye kila nyanya ya utekelezaji wa mradi huu.
Refocus Africa imeanza kuwekeza kwenye nchi zaidi ya 12 kwenye sekta ya kilimo, madini, elimu, majengo, sanaa na michezo, Kampuni hii imesajiliwa pia Tanzania na Makao Makuu yake yapo Zanzibar ambapo mwaka 2021 walifanikiwa kuwasilisha mipango yao ya uwekezaji kwa Rais wa Zanzibar Dr Hussein Ally Mwinyi lakini kutokana na changamoto ya ufinyu wa maeneo ya kuwekeza Zanzibar wakaamua wawekeze Pangani ambako jiografia yake inafanana na Zanzibar.