Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sirro awapa vyeo walioua majambazi

34347 Pic+sirro Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali (IGP), Simon Sirro amewapandisha vyeo askari watano wa jeshi hilo mkoani Mwanza pamoja na kuwapatia Sh200, 000 kila mmoja kama motisha na zawadi kwa umahiri na ujasiri wao wa kupambana na matukio ya uhalifu ikiwamo ujambazi jijini Mwanza.

Kupandishwa vyeo kwa askari hao ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alipotembelea mkoa wa Mwanza Novemba 23, 2018 baada ya kupokea taarifa ya mapambano ya dakika 45 kati ya askari polisi na watu waliotuhumiwa kuwa majambazi yaliyotokea usiku wa kumkia Novemba 15, mwaka jana.

Katika tukio hilo, watu saba wanaotuhumiwa kuwa majambazi waliuawa huku askari polisi mmoja akijeruhiwa mguuni.

Waliotunukiwa na vyeo vyao vipya kwenye mabano ni Amon Rubanzibwa (Stafu Sajenti), Belson Sanga (Sajenti) na Rodrick Ndyamukama, Thomas Masingija na mwanamke pekee Dominika Nnko ambao wote wametunukiwa ukoplo.

Akiwavisha vyeo vipya askari hao watano katika hafla iliyofanyika kambi ya polisi Mabatini jijini Mwanza, Kamanda wa polisi mkoa huo, Jonathan Shanna aliwataka askari hao kutumia zawadi hiyo kama chachu ya kuongeza bidii na weledi wakati wa kutimiza majukumu yao.

“Kupandishwa vyeo hasa kwa askari wa kike walioweza kupambana na kukabiliana kikamilifu na majambazi kuwe ni chachu ya kuongeza bidii, weledi na ufanisi kazini,” alisema Kamanda Shanna.

Naye mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo aliwazawadia askari hao fedha taslimu Sh 1.3 milioni pamoja na vyeti vya umahiri kazini.

Mmoja wa askari hao, Dominica Nnko kwa niaba ya wenzake alishukuru kwa kupandishwa cheo na zawadi walizopewa, huku akiahidi kuongeza juhudi, maarifa na weledi katika utendaji wao wa kusimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao.



Chanzo: mwananchi.co.tz