Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri ya wana Kilimanjaro kuzika kwenye vihamba

28308 Kill+pic TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ya kutaka kutengwa maeneo ya maziko katika Mkoa Kilimanjaro imeibua mjadala huku suala la kuenzi mila likitajwa kuwa ni sababu ya kuzika kwenye vihamba.

Baadhi ya wananchi wa Kilimanjaro waliohojiwa na Mwananchi wamesema, kimila ni lazima marehemu azikwe kwao ambako kitovu chake kilizikwa, tofauti na hivyo huleta balaa kwa familia.

Wakazi wa hao Wachaga wa wilaya za Rombo, Hai, Moshi na Siha, wana utamaduni wa enzi na enzi wa kuzika ndugu zao katika mashamba madogo ya maeneo yao ya asili maarufu ‘vihamba’.

Lakini wiki iliyopita Waziri Lukuvi aliziagiza halmashauri zote za mkoa huo, kutenga maeneo ya jumuiya kwa ajili ya maziko, ili wakazi wa mji huo waone umuhimu wa kuzika kwenye makaburi hayo.

Mangi Marealle, wadau wafichua siri

Kiongozi wa Kimila ambaye ni Mangi wa Wachaga wa Marangu, Frank Marealle, alisema sababu ya wakazi wa maeneo ya uchagani kuzika kwenye vihamba ni mila na desturi za kabila hilo.

Mangi Marealle ambaye alimrithi Chifu Agustino Marealle aliyefariki dunia mwaka 2006, alisema kwa mila za Wachaga, mtoto wa kwanza na wa mwisho katika familia lazima wazikwe kwenye kihamba.

“Hizi ni mila tu kwamba kwa mfano ukiwa na watoto watatu. Yule wa kwanza na wa mwisho ndio wanagawiwa kihamba kila mmoja. Kama eneo litabaki ndio atapewa huyo wa katikati,” alisema.

Alisema watoto hao wanapokufa, huzikwa katika vihamba vyao lakini kwa sasa kuna shida kutokana na uhaba wa maeneo, na wanatafakari mustakabali wa siku za usoni.

“Tunafikiria tuachane na huu utaratibu au tuendelee kuzika,” alisema na kueleza kuwa hata agizo la Lukuvi litapata changamoto ya maeneo ya kuzikia.

Mkazi wa Machame, Basil Lema alisema mtoto anapozaliwa, kitovu chake hakitupwi ovyo, lazima kizikwe kwenye eneo la familia na ndipo pia atakapozikwa.

“Hata kama mtoto amezaliwa New York (Marekani), lazima ukitunze hicho kitovu na kukirudisha huku nyumbani na kuna mila zake, ni lazima hapo kinapozikwa paoteshwe mgomba,” alisema Lema.

Hata hivyo, Lema alisema katika siku za karibuni, waumini wa Kikristo walianza kuzika katika maeneo ya jumuiya ya kanisa ambayo nayo yamejaa na sasa baadhi wamerudi kwenye vihamba.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Shirimatunda, Beda Massawe, alisema utaratibu wa kuzika kwenye vihamba wameukuta na upo tangu enzi za mababu, na wao wamerithi kama mila na kuiendeleza.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alisema ofisi yake ina maeneo matatu kwa ajili ya maziko.

“Tuna maeneo Karanga, Njoro na Pasua na hapo Bondeni karibu na TBL na tumenunua eneo lingine huko Mtakuja Moshi Vijijini.”

Alisema sheria za manispaa zinazuia mtu kuzikwa katika eneo lake lililopimwa isipokuwa kwa kibali maalumu.

Mwandezi alisema maeneo ambayo watu huzika kwenye vihamba ni yale yaliyo nje ya manispaa hiyo na ambayo hayajapimwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz