Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri migogoro ya fidia yatajwa

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kahama. Imeelezwa kuwa idadi kubwa ya wananchi waishio maeneo ya uwekezaji katika sekta ya madini hawana uelewa wa malipo ya fidia hali ambayo huchangia kuwapo kwa migogoro mingi kati ya wawekezaji na jamii inayowazunguka.

Hayo yalielezwa kwenye kikao cha majadiliano kati ya maofisa kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Biashara na asasi zisizo za kiserikali kilichofanyika mjini Kahama mkoani Shinyanga juzi.

Ofisa Msaidizi wa Miradi wa Haki za Binadamu na Biashara wa kituo hicho, Tito Magoti alisema tatizo la uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na suala hilo kumechangia migogoro mingi kutokana na idadi kubwa ya wawekezaji kwenda kwenye maeneo ya watu na kuchukua ardhi wakiwa na vibali kutoka serikalini.

Alisema kutokana na wananchi kutokuwa na uelewa hupewa fidia kidogo ambayo kwa wakati huo hudhani ni kubwa lakini baada ya kugundua kwamba ni kiduchu huanza kudai fidia upya na hapo ndipo huibuka migogoro.

“Ili kumaliza migogoro hii hatuna budi kutoa elimu ya sheria ya ardhi kwa wananchi ili wawe na uelewa wa kutosha wa masuala ya fidia hasa katika wilaya ya Kahama ambayo imezungukwa na madini mengi ambayo wawekezaji hufika kwa ajili ya kuwekeza migodi mikubwa na midogo,” alisema Magoti

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Serikali za mitaa katika mtaa wa Mwime katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, Charles Kazobya alisema tatizo lililopo siyo la wawekezaji, bali ni la baadhi ya viongozi wa Serikali ambao hujiweka katikati ya mwekezaji na wananchi kwa maslahi binafsi.

Naye Paul Ntelya kutoka taasisi ya umoja wa wazee Kahama, alisema tatizo lililopo ni viongozi wa Serikali kuwanyima haki ya kujua sheria ya ardhi na fidia ili watumie fursa hiyo kuwanyanyasa na kuwadhulumu fidia.

Ntelya aliwataka watetezi wa haki za binadamu kufika mara kwa mara kwa wananchi kutoa elimu hiyo na kuwakutanisha na viongozi wa Serikali ili kuondoa hali hiyo.

Kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro mingi katika maeneo yenye madini kati ya wananchi na wawekezaji kutoka na ama wananchi waliokuwa wakiishi ama kufanya uchimbaji mdogo katika maeneo hayo kuondolewa bila ya kulipwa fidia au kulipwa fidia kiduchu jambo ambalo hawakubaliani nalo.

Migogoro hiyo wakati mwingine huibua uhasama mkubwa kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi na wakati mwingine hutokea matukio ya wananchi kuuawa ama kujeruhiwa katika migogoro hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz