Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sinunuliki mtaji wangu wananchi

10226 SUGU+PIC TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema hakuna mtu anayeweza kumnunua ili akihame chama hicho kwa kuwa mtaji wake ni wananchi waliomchagua na si fedha.

Akizungumza jana jioni Agosti 4, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uyole mjini hapa, Sugu pia aliwashukia wanasiasa wanaopita katika jimbo lake na kumchafua, kubainisha kuwa Mbeya si sehemu ya ajira ya wanasiasa uchwara.

Amesema yupo tayari kufa kwa ajili ya kuwapigania wananchi wa Mbeya na kamwe hawezi kuwasaliti, “kwenye mitandao ya kijamii eti inaelezwa imetengwa Sh2bilioni kwa ajili ya kumnunua Sugu. Niwaeleze tu kuwa sina bei.”

“Nimeshadhulumiwa mambo mengi sana kuliko hizo Sh2bilioni. Ukitaka kuninunua mimi hakikisha umetupanga foleni wana Mbeya wote na uanze kumnunua wa kwanza na mimi nitakuwa wa mwisho kama hazitakutoka mbio.”

Amesema, “Tuna kazi  ya kuliokoa hili Taifa na tupo tayari kuifanya kazi hiyo kwa gharama yoyote ile. Mtu akishakupeleka gerezani anachokuwa amebakiza ni kukupeleka kaburini kwa hiyo mimi sina cha kupoteza na nipo tayari kufa kwa ajili ya Mbeya na siogopi chochote.”

Awali, mratibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga amesema demokrasia inazidi kuporomoka nchini hivyo Watanzania wanahitaji kuamka na kuipigania.

Amesema kuanzia Septemba 9, 2018 ataanza kuzunguka katika majimbo ya Chadema kanda ya nyanda za juu kusini kufanya mikutano.

Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, Obadia Mwaipalu amesema hakuna mtu yeyote mkubwa zaidi ya chama, kwamba uamuzi waliochukua kuwavua uanachama madiwani wao wanne ulikuwa na baraka zote, kwa maelezo kuwa walikuwa watovu wa nidhamu.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz