Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sintofahau ajira ya Ester baada kukatwa vidole

Vidole Pic Ester Mkombozi, aliyekatwa vidole vyote vitano vya mkono wa kushoto baada ya kuchomwa sindano

Thu, 25 May 2023 Chanzo: Mwananchi

Hatimaye Mkazi wa Arusha Ester Mkombozi (34) aliyedai kuchomwa sindano katika duka la dawa muhimu na baadaye ‘kuungua’ vidole vya mkono wa kushoto, ameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kukatwa vidole hivyo na kubaki na kiganja.

Ester aliyedai kupata masahibu hayo baada ya kuchomwa sindano katika duka la dawa lililopo eneo la Ngulelo mkoani hapa, amekatwa vidole hivyo Mei 8, 2023 katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru alipokuwa amelazwa tangu Mei Mosi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, Ester amesema kuwa baada ya kulazwa kwa wiki moja hospitalini hapo, alilazimika kufanyiwa upasuaji na kukatwa vidole vyote baada kuelezwa sumu ilikuwa imesambaa.

“Nakumbuka Machi 20 mwaka huu nilikuwa na dalili za ugonjwa wa ‘UTI,’ nikaenda pale duka la dawa nikapimwa na majibu yakaonyesha ninayo. Hivyo yule mama alinianzishia sindano, na tangu anichome; hali yangu ilibadilika hadi kufikia hatua hii ya kukatwa vidole vyote,’ amesema.

“Baada ya kuugua kwa zaidi ya mwezi mmoja na wiki, hali yangu ilizidi kuwa mbaya majirani zangu walinipeleka Mt Meru na nikalazwa pale kwa muda wa wiki moja kabla sijafanyiwa operesheni hii Mei 8, mwaka huu ambapo niliambiwa sitaweza kupona pasipo kukatwa vidole maana sumu iliendelea kutembea,” amesema.

Kwa upande mwingine, Ester amesema: “Nikiwa hospitali, nilipata matibabu mazuri na ninamshukuru Mungu alitoka salama na maumivu yamepungua. Leo ndiyo nimetoka hospitali, nashukuru serikali na watu wengine kwa kunisaidia ikiwemo majirani zangu,”

Aidha Ester ambaye ni mama wa watoto wawili na aliyekuwa akijishughulisha na ususi, amewataka wananchi kuhakikisha wanapohisi kuugua, vi vema kuwahi hospitali kwani yeye binafsi angewahi na kupata matibabu sahihi, asingefikia hatua aliyopo sasa.

“Kabla sijaletwa na majirani zangu hospitali, kuna mtu aliniambia kuna nabii mahali anaombea na niliponenda kwa yule nabii aliniambia niende na sadaka ya Sh 50,000 ambayo licha ya kuipeleka na kufanyiwa maombi sikupata nafuu na aliniambia niendelee kwenda na siku iliyofuata alinitaka niende na maji, asali, na sabuni,” amedai Ester na kuongeza.

Ester anaamini kilichomtokea hakikuwa jambo la kawaida.

“Mimi kosa nilifanya kuchelewa matibabu na ndiyo linanifanya nijute, kwa maisha niliyonayo nategemea sana mikono yangu kujipatia mahitaji yangu kama vile kodi, na chakula kwa watoto, sasa kwa hali hii; sielewi naanzia wapi,” amesema.

Awali Dk Amani Kiruu kutoka Kitengo cha Upasuaji hospitalini hapo ameeleza kuwa kilichotokea ni vidole vya mkono kuharibika, na kwamba hakukua na matibabu mengine yanayoweza kufanyika zaidi ya kufanya upasuaji na kuondoa hiyo sehemu ya vidole vilivyoharibika.

“Tatizo kama hili sababu ni nyingi inaweza ikasababishwa na mishipa ya damu inayosambaza damu sehemu mbalimbali za mwili kuzibwa, hivyo sehemu ya mwili isipopata damu kwa muda mrefu inafikia hatua inaharibika na ndicho kilichotokea kwa mgonjwa wetu,” amefafanua.

Kwa mujibu wa daktari huyo, ni kwamba maelezo ya mgonjwa yaliwafanya washindwe kujua chanzo cha tatizo japo kisababishi ni damu hatofika kwenye vidole na hivyo kuharibika.

“Ningependa niwashauri wananchi wanapojisikia utofauti, wasiende duka la dawa pasipokuwa na cheti cha daktari chenye kuonyesha ugonjwa na dawa; hivyo ni budi kwanza waende hospitali na huko watafanyiwa vipimo ambavyo vitatoa majibu ya ugonjwa na baadaye kupata matibabu sahihi,” ameongeza Dk Kiruu.

Kwa upande wake Anna Laizer, Muuguzi anayedaiwa kumchoma sindano hiyo; alikana kumchoma na kudai kuwa hawezi kumchoma mgonjwa sindano bila kuonyeshwa cheti cha daktari.

Hivi karibuni Mamlaka ya Dawa na Vitaa Tiba Tanzania (TMDA), imesema inafanya uchunguzi wa tukio hilo na itatoa taarifa kamili.

Chanzo: Mwananchi