Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sintofahamu mwili wa mwanamke uliozikwa kando mwa barabara wafukuliwa

Makaburi Mes Sintofahamu mwili wa mwanamke uliozikwa kando mwa barabara wafukuliwa

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwili wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 na 40 umeokotwa ukiwa umetelekezwa kando mwa barabara kuu ya Moshi – Arusha, eneo la Kwa Msomali, kitongoji cha Darajani.

Kitongoji hicho ambacho kipo katika kijiji cha Sanya Station, kipo wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Mwili wa mwanamke huyo ambao haujajulikana wala eneo alikouawa, uliokotwa jana Jumapili, Januari 28, 2024, ukiwa umeharibika kiasi cha kutoa wadudu.

Baadhi ya watu waliozungumza na Mwananchi Digital, wanadai Jeshi la Polisi liliamuru mwili huo uzikwe mita chache ndani ya hifadhi ya barabara kabla ya kufukuliwa jioni ya leo Januari 29, 2024.

Awali alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kujua ni kwa nini mwili huo haukondelewa eneo la tukio mpaka hapo ulipozikwa eneo la hifadhi ya barabara amesema, mwili kuchukuliwa eneo la tukio inategemea upo katika hali gani.

"Suala la kuchukua mwili inategemea upo katika hali gani, polisi walienda eneo la tukio na daktari akawa amechukua baadhi ya sampuli za vipimo vya DNA kutokana na kwamba mwili ulikuwa hauwezi kuhifadhiwa kwa hali ulivyokuwa," amesema.

Baadaye alipoulizwa ni kwa nini mwili umefukuliwa, Kamanda Maigwa amesema baada ya polisi kufanya taratibu zote waliukabidhi mwili kwa Serikali ya kijiji na wao ndio waliouzika lakini baadaye ilibainika umezikwa kimakosa.

"Tuliomba kibali cha Mahakama kuufukua mwili maana uongozi wa serikali ya kijiji ulizika kwenye hifadhi ya barabara kimakosa, hivyo mwili umechukuliwa na kwenda kuzikwa makaburi ya Kimaroroni," amesema Kamanda Maigwa.

Wakizungumza awali, baadhi ya mashuhuda wamesema mwili wa mwanamke huyo ulianza kuonekana Jumamosi Januari 27, 2024 usiku ukiwa umeharibika, ukitoa wadudu.

Mwananchi Digital ilipofika eneo hilo leo Jumatatu, Januari 29, 2024, ilikuta mwili umeshazikwa lakini eneo hilo likiwa bado lina harufu kali.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Darajani, Rabson Mbasha amesema mwili huo waliukuta tayari umeshaharibika kiasi cha hata sura kutojulikana.

"Juzi nilikuwa kwenye shughuli zangu za kilimo, nilirudi nyumbani saa nne kasorobo usiku, nilipigiwa simu na jirani ambaye ni balozi wa mtaa, akaniambia kuna mwili umetupwa eneo la barabarani umeshaoza, hivyo nilifika eneo hilo usiku huohuo na kuuona,” amesema.

“Niliwapigia simu polisi nao wakafika muda huohuo, walipouona wakasema hawawezi kuuchukua kwa sababu ulikuwa umeshaharibika na hata sura haionekani, wakaniambia tuuache palepale mpaka kesho yake ili tuone namna ya kufanya na ikiwezekana tuuzike hapahapa,” amesema.

Amesema jana Januari 28, 2024 polisi walifika eneo hilo na wakaukuta mwili jinsi walivyouacha.

‘’Wakatuambia tutafute wananchi ili tuuzike kwa amri yao, wananchi kweli walijitokeza wakachimba kaburi hapo pembeni tukauzika ule mwili asubuhi," amesema.

Alipoulizwa iwapo kuna fufunu zozote kama mtu huyo anafahamika, amesema: “Mwanamke huyo bado hajafahamika ni wa wapi na alitolewa wapi mpaka tumemzika hapo tulipomuokota.”

Balozi wa eneo hilo, Peter Sangale, alikiri mwili wa mwanamke huyo kutupwa eneo lake.

"Nilipata taarifa kutoka kwa wenzangu kwamba kuna mwili uko pembezoni mwa barabara umetupwa na umeharibika, tulienda eneo la tukio. Tulipofika mwenyekiti akatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama na walifika eneo la tukio. Walipofika walishauri mwili ule uachwe pale mpaka kesho yake kwa sababu ulikiwa umeharibika, hivyo tuliuacha pale mpaka asubuhi walipofika na kuamuru uzikwe palepale.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live