“Kama isingekuwa uzembe na kuachwa kwa muda mrefu bila kupata huduma mtoto wangu angekuwa hai, wangenihudumia tangu asubuhi nilipofika yasingetokea haya. Zakhiem ni hospitali nzuri, lakini ina shida kubwa.”
Hiyo ni kauli ya Nailath Lyezia, mkazi wa Mbande, Dar es Salaam anayelalamikia watoa huduma katika hospitali ya Mbagala Rangitatu kusababisha kifo cha mtoto wake dakika chache baada ya kujifungua kwa kukaa saa 15 bila huduma, huku nyaraka zilizotolewa Mei 24, 2023 zikionyesha mtoto huyo alifia tumboni akiwa na miezi minane.
Hata hivyo utata umeibuka, hali iliyomlazimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke kuunda timu kuchunguza ukweli wa malalamiko hayo yanayokinzana na taarifa zinazotolewa na uongozi wa hospitali ya Rangitatu.
Akizungumza nasi jana nyumbani kwao, Nailath alisema alifika hospitalini hapo saa 12 asubuhi na kuanza taratatibu za usajili kupitia dirisha la bima alizozikamisha saa mbili na kisha akaenda kliniki alikoanza kufanyiwa vipimo.
“Nesi aliyenipima alibaini kuwa mapigo ya moyo ya mtoto yako chini, akanielekeza niende kwenye kipimo cha Ultra Sound. Huko nako nilifanyiwa ambacho kilithibitisha kulikuwa na tatizo, hivyo aliyenipima akaniambia niwahi kumnusuru mtoto, akanipeleka leba na kuwaambia wahusika kwamba nahitaji kuangaliwa kwa dharura,” alisema Nailath.
Alisema baada ya subira ya muda mrefu, hatimaye aliruhusiwa kuingia. “Nilipoingia akaniambia nipande kitandani halafu yeye akatoka nje, nilikaa kwa nusu saa bila kupata huduma yoyote, aliponipima na yeye akaniambia kwa hali niliyonayo mambo mawili yanaweza kutokea, nayo ni kupata au kukosa mtoto.
“Baada ya hapo nikaambiwa niingie leba ambako niliandikiwa dawa, nilikwenda na ile karatasi ya dawa kwa mume wangu ili akafuatilie dawa,” alisema.
Hata hivyo, alisema mumewe alipofika kwenye dirisha la dawa akaambiwa bado mkewe hajaingizwa kwenye mfumo wa bima na hata alipokwenda kwa watu wa bima alianza kuzungushwa.
“Niliporudi chini kwenye dawa jibu likawa lile lile bado hawajaingiza, nikapanda tena juu manesi wakawa wananifokea lakini safari hii ikawa tayari wameshaniingiza kwenye mfumo,” alisema.
Baada ya kupata dawa alirejea leba, lakini uvumilivu wake ulimuweka katika hospitali hiyo kwa saa takribani saa 15 bila kupata huduma yoyote hadi ilipofika saa 4 usiku ndipo alipoanza kuhudumiwa kwa kuchomwa sindano ya uchungu.
“Nesi aliyenizalisha alinionyesha mtoto wangu na akamuweka kifuani, baada ya muda mfupi akaniambia amefariki,” alisema Leilath huku akibujikwa na machozi.
Kauli ya mume
Wakati Nailath akieleza hayo, mumewe, Hassan Mapunda anasema alishapewa taarifa za kifo cha mtoto wao akiwa tumboni tangu saa 10 jioni.
“Baada ya kusota kutwa nzima hatimaye saa 10 jioni nilipata taarifa kutoka dawati la malalamiko kwamba mtoto amefia tumboni, kilichonishangaza hivi inawezekanaje mtu mwenye hali hiyo akaachwa bila kuhudumiwa hadi saa nne usiku?
“Kingine mhusika mwenyewe anasema alimsikia mtoto akilia mara moja wakati anajifungua, na alijifungua saa nne usiku, sasa iweje mie niambiwe kuwa alifariki tumboni?” alihoji Mapunda.
Hospitali yafafanua
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mbagala Rangiatu, Dk Ally Mussa akizungumza na Mwananchi alikiri Nailath kuhudumiwa katika hospitali hiyo katika tarehe husika, huku akikanusha madai kwamba alijifungua mtoto akiwa hai.
“Ni kweli alihudumiwa hapa na alikuja kutokana na kutomsikia mtoto akicheza, alipofanyiwa Ultra Sound ikaonekana mtoto amefia tumboni na aliambiwa tangu asubuhi. Ilishajulikana haikuwa dharura, walihudumiwa wagonjwa wengine wa dharura.
“Si kwamba aliachwa bila huduma, inawezekana hakujua kama anahudumiwa, ila saa 12 alipewa dawa ya kidonge akameza. Ile ilikuwa inamsaidia kumtengenezea njia ya kujifungua, muda wote huo aliokuwa hospitali alikuwa anahudumiwa kama mama ambaye mtoto amefia tumboni,” alisema.
Hata hivyo, Nailath alipinga majibu akisema, “hakuna dawa yoyote niliyopewa hadi saa nne usiku, halafu kama wanasema mtoto alifia tumboni kuanzia asubuhi kwa nini sikuambiwa? Kwa nini yule mtu wa ultra sound aniambie wahi umuokoe mtoto?
“Je, ni sahihi kwa mjamzito ambaye mtoto wake amefia tumboni tangu asubuhi kuachwa kutwa nzima bila huduma, vipi kuhusu usalama wangu? Nikiwa pale alikuja mwanamke mwingine ambaye mtoto wake alifia tumboni, kwa haraka alifanyiwa upasuaji, kwa nini mimi sikuhudumiwa?” alihoji.
Akizungumzia sakata hilo, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini halmashauri ya Temeke, Francisca Elimo alisema ofisi ya mganga mkuu imepata taarifa kuhusu malalamiko hayo, ingawa kuna mkanganyiko wa taarifa.
“Mganga mkuu ameunda timu ya kufuatilia hili na taarifa tutaitoa baada ya kumaliza kazi yake, kwa sasa tutahitaji ushirikiano kutoka kwa familia hiyo,” alisema Fransisca.