Jeshi la Polisi nchini limesema taarifa za kuuawa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wilayani Missenyi mkoani Kagera, Joseph Remigius (52) si za kweli na zinalenga kuupotosha umma.
Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime kupitia taarifa kwa umma ameeleza hayo leo Ijumaa Novemba Mosi, 2024.
Awali kupitia mitandao ya kijamii zilisambaa taarifa za kifo cha kada huyo ambaye pia alitia nia kugombea uenyekiti wa Kijiji cha Karagara wilayani humo, huku sintofahamu ikiibuka akidaiwa kuuawa.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa Chadema mkoani Kagera, Daniel Damian amesema bado wapo katika sintofahamu juu ya kifo cha kada wao kutokana na mkanganyiko wa taarifa.
"Nashindwa kutoa taarifa ambazo sina uhakika nazo zaidi kwa sababu viongozi wangu wa kata wana taarifa zinatoafutiana kuhusu marehemu, nashindwa niseme nini mara alikuwa amelewa, mara aligongwa na bodaboda mara aliuawa halafu akategeshewa barabarani," amesema.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Misime imesema: “Tumeshuhudia kupitia mitandao ya kijamii ikitolewa taarifa ya kutaka kuupotosha umma kuhusiana na kifo cha Joseph Remigius, mkazi wa Kijiji cha Karagara, Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera ambaye alikuwa ametia nia ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji kupitia Chadema.
“Taarifa sahihi ni kwamba Oktoba 31, 2024 Joseph Remigius majira ya saa tatu usiku akiwa anatoka kwenye baa waliyokuwa wanakunywa pombe akiwa amebebwa na bodaboda walipata ajali na baada ya ajali hiyo walipata msaada na kufikishwa katika Kituo cha Afya Minziro na kupatiwa matibabu na kuruhusiwa.”
Katika taarifa hiyo, Misime amesema leo Novemba mosi, 2024 saa 10.20 alfajiri ndipo zikapokewa taarifa katika Kituo Kidogo cha Polisi Minziro kuwa Joseph Remigius amefariki dunia akiwa nyumbani kwake.
“Hivyo hadi sasa kulingana na ushahidi wa mashuhuda wa ajali na waliompatia msaada na kumfikisha katika Kituo cha Afya Minziro, ajali ndiyo chanzo cha kifo chake. Endapo kuna mwenye ushahidi tofauti na huo wa mashuhuda wa ajali basi aufikishe polisi ili ufanyiwe kazi,” imehitimisha taarifa hiyo.