Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sintofahamu Moshi kuwa jiji, Mbunge amwangukia Rais

Moshi View Kilimanjaro Sintofahamu Moshi kuwa jiji, Mbunge amwangukia Rais

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Je, ndoto ya Moshi kuwa jiji itatimia mwaka 2024? Ndilo swali wanalojiuliza wananchi wa mji huo, baada ya mchakato huo kuchukua zaidi ya miaka 10 licha ya kutimiza vigezo vyote, huku Mbunge, Priscus Tarimo akimwangukia Rais Samia Suluhu.

Mwaka 2012, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliziagiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi (MMC) na ile ya Moshi (MDC) kukaa meza moja kuhakikisha zinaondoa toafuti zao, ili mji huo upande hadhi na uwe Jiji ifikapo mwaka 2015.

Kauli ya Kikwete wakati huo, ilitokana na aliyekuwa Mkurugenzi wa MMC wakati huo, Bernadetta Kinabo kuwashitaki wenzao wa MDC, akidai wamekuwa kikwazo kwa mji huo kuongeza eneo kutoka kilometa za mraba 58 hadi 126 kuelekea MDC na Hai.

Hata hivyo, tofauti hizo zilimalizika na mwaka 2016, Serikali ilitangaza GN namba 219 iliyochapishwa kwenye gazeti la Serikali na kutiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, ikiongeza eneo la mji huo kutoka kilometa za mraba 58 mpaka kufikia kilometa za mraba 126.

Waziri Lukuvi kupitia tangazo la Serikali (GN) namba 219 la Julai 15, mwaka huo, na nakala yake kusambazwa kwa watendaji, madiwani na wananchi, vitongoji katika vijiji 10 vya wilaya hizo mbili, liliingizwa eneo hilo la Moshi mjini.

Kwa mujibu wa GN hiyo, vitongoji hivyo 40 vipo katika kata za Oldmoshi Magharibi, Kimochi, Kindi, Mabogini katika wilaya ya Moshi na kata ya Machame Kusini iliyopo wilaya ya Hai hivyo kigezo cha ukubwa wa eneo kikafikiwa.

Pamoja na kutimiza vigezo hivyo, lakini baada ya Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015, alitembelea mji huo na alisitisha mchakato huo baada ya mwananchi mmoja kulalamikia kuporwa ardhi.

Mbunge, wananchi waibua kilio

Januari 22, 2024, Mbunge wa Moshi mjini, Priscus Tarimo aliwasilisha kilio cha Moshi kuwa jiji kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda alipofanya mkutano stendi kuu ya mabasi, ingawa hakutoa kauli yoyote.

Akizungumza na gazeti hili leo Jumatatu Januari 29, 2024, mbunge huyo amesema kwa hapo walipofikia, kiongozi pekee anayeweza kuukwamua mchakato huo ukamilike ni Rais, kauli ambayo imeungwa mkono na baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti.

“Kwa hapa tulipofika kwa sababu GN ilishatoka, ni Rais tu (Magufuli) alisema tusubiri. Bahati nzuri mamlaka haya yako kwa Rais, tunaamini ndiye pekee anaweza kutukwamua kwa kutoa neno moja tu kuwa mchakato ule ukamilike,”amesema Tarimo na kuongeza:

“Akisema hivyo tu, sisi tutakamilisha kwa sababu hatua zote za ramani, makubaliano na vikao vimeshakamilika. Sasa hivi tunamuomba mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan abariki mchakato ule tuwe jiji la kisasa.”

Baadhi ya wananchi wa mji huo, wanasema suala la Moshi kuwa jiji lilikuwa moja ya ahadi za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kikiwaahidi wananchi kuwa kina uwezo wa kulishughulikia suala hilo.

Baraka Ansbert ambaye ni dereva wa malori ya mchanga katika mji huo, anasema kama mji huo hautakuwa jiji kati ya sasa hadi kufikia uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofayika mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2025, basi CCM na Serikali zije na majibu yanayoeleweka.

“Tunaibana CCM kwa sababu walitumia hili suala kama turufu yao katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwamba, oooh Chadema hawawezi kwa sababu hawana Serikali. Sasa tuliwapa kura na wao ndio wako madarakani, mbona hautuoni jiji,” amehoji.

Magdalena Ambros ambaye ni mjasiriamali wa viatu na mabegi ya mtumba, anasema anavyosikia kila kitu kilikwenda vizuri hadi mwaka 2017 uliposimamishwa na Rais aliyekuwa madarakani kwa sababu ambazo bado hazijawekwa wazi.

“Mimi niliwahi kumuuliza Meya wa wakati ule, Raymond Mboya nini kimetokea akasema alivyoelezwa kuna mchungaji alilalamika kwa Magufuli kuwa wanaporwa ardhi yao. Lakini kumbuka kila kitu kilikwenda sawa hadi GN ikatoka,”anadai Magdalena.

“Kwa sababu aliyeuzuia huu mchakato ni Rais, basi tunamuomba Rais Samia atufungue hii minyororo maana kama ni kura tuliwapa 2020 sasa tatizo ni nini? Au ndio ile hisia wanayotuona kuwa Kilimanjaro ni wapinzani?”alihoji Magdalena.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi anasema jambo hilo bado liko kwenye mchakato na wao kama chama wako mstari wa mbele kuhakikisha ndoto ya wana Moshi inatimia ili kuchochea zaidi maendeleo ya mji.

“Kwa kweli tunalifuatilia na kuna vigezo ambavyo tulielekezwa kuvizingatia. Moja ni kiwango cha mapato, pili ni ukubwa wa eneo na tatu ni idadi ya wakazi wake. Yote haya yanafanyiwa kazi kwa ushirikiano na Halmashauri na Serikali,”amesema Boisafi.

Jitihada za kumpata mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe kuzungumzia suala hilo ambalo liliibuliwa pia katika mkutano wa Makonda hazikufanikiwa baada ya kutopatikana kwa simu alipotafutwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live