Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida kuna gari moja la Zimamoto

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Bunge limeelezwa leo kuwa mkoa wa Singida una gari moja tu la Zimamoto ambalo nalo ni bovu.

Hayo yameelezwa  bungeni leo Septemba 5 na Mbunge wa Viti Maalumu Aisharose Matembe  (CCM) ambaye amesema gari hilo ni bovu na linahudumia wilaya zote za mkoa wa Singida.

Mbunge huyo ameomba kujua ni lini zimamoto watapatiwa gari jingine.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Hamad Masauni amekiri mkoa huo kuwa na gari moja la Zimamoto lenye ujazo wa lita 1500 ambalo amesema linafanya kazi vyema.

"Gari hilo ni zima na linafanya kazi vizuri lakini la pili ndilo bovu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatarajia kufanya matengenezo ya gari la pili lenye ujazo wa lita 7,000 pindi fedha zitakapopatikana," amesema Masauni.

 

Naibu Waziri huyo ameliambia Bunge leo kuwa, shughuli za zimamoto na uokoaji zitaendelea kuimarishwa na katika bajeti ya 2018/19 Serikali imepanga kununua magari mengine na kuyagawa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu wilaya amesema Wizara inaandaa marekebisho ya sheria ya zimamoto na uokoaji ya mwaka 2007, ili wilaya ziruhusiwe kununua magari yao ya zimamoto jambo ambalo litapunguza tatizo hilo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz