Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi za wanafunzi bora zenye furaha, majonzi

91507 Wanafunzi+pic Simulizi za wanafunzi bora zenye furaha, majonzi

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Ni simulizi za furaha zinazoambatana na huzuni kutoka kwa wahitimu waliomo katika orodha ya wanafunzi 10 bora katika Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2019.

Hiyo ni kutokana na baadhi kulazimika kuvumilia kusoma katika hali zote ili kufanya vizuri katika mitihani yao.

Simulizi hizo za baadhi ya vinara hao walizitoa jana ikiwa ni siku moja tu baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza matokeo hayo huku wanafunzi 10 bora, saba wakiwa ni wasichana. Sita kati ya 10 wanatoka shule moja ya St Francis ya Mbeya.

Wanafunzi hao wakiongozwa na Joan Ritte wa St Francis Girls ni Denis Kinyange (Nyegezi Seminary- Mwanza), Erick Mutasingwa (Sengerema Seminary-Mwanza), Rosalia Mwidege, Domina Wamara wote wa St Francis Girls, Mvano Cobangoh (Feza Boy’s-Dar es Salaam), Agatha Mlelwa, Sarah Kaduma, Shammah Kiunsi wote wa St Francis Girls na wa kumi ni Lucy Magashi wa Huruma Girls ya Dodoma.

Akitangaza matokeo hayo juzi, katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema watahiniwa wa shule 340,914 sawa na asilimia 80.65 ya watahiniwa 422,722 wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 175,296 sawa na asilimia 79.46 na wavulana ni 165,618 sawa na asilimia 81.94.


“Yeye ni mwalimu wa shule ya msingi na kuna ndugu zangu watatu walionitangulia anawasomesha yeye ni kama nilianza kupoteza matumaini,” anasema Domina Wamara mhitimu wa St Francis aliyeshika nafasi ya tano

Anasema kuna wakati alilazimika kuvumilia alipokosa mahitaji muhimu kwa wakati huku akimtaja mama yake, Magreth Augustine kuwa mtu pekee aliyekuwa akihangaika.

“Shule yetu ilikuwa inajua nalelewa na mzazi mmoja hivyo ilikuwa ni ngumu kunidai ada au kunirudisha nyumbani bali kunivumilia hadi ninapomaliza,” anasimuliza Domina mwenye miaka 17 mwenye ndoto za kuwa daktari bingwa wa upasuaji

Wakati Domina akieleza hayo, mama yake mzazi, Magreth anaonekana bado hajaamini kilichotokea huku akitaja shida alizopitia kumsomesha binti yake. “Baba yao alifariki ghafla kwa kupigwa na majambazi Aprili 2014 jambo lililonifanya kubeba majukumu yote ikiwamo kuwasomesha, ilikuwa shida, nililazimika kuingia katika mikopo benki, saccos na kujishughulisha na biashara.”

“Hata shule aliyomaliza aliomba nimpeleke nikawa na wasiwasi kutokana na ada ya shule hiyo nisingeweza kuimudu ila aliniahidi atafanya vizuri ndiyo hii zawadi aliyonipatia amenifurahisha sana mwanangu,” anasema Magreth.

Matokeo yamkumbusha kifo cha baba yake

Wakati wengine wakipokea matokeo hayo kwa furaha, hali imekuwa tofauti kwa Mvono Cabangoh (18) aliyehitimu Feza Boy’s na kufanikiwa kushika nafasi ya sita kwa kumkumbusha kifo cha baba yale, Philip Cabangoh aliyefariki mwaka 2017 angekuwapo ili ashuhudie matokeo hayo.

“Lazima nikubali nilifurahia sana haya matokeo, lakini wakati huo huo nilikuwa na huzuni maana nilitamani baba yangu angekuwa hai kushuhudia wakati huu mzuri katika maisha yangu,” anasema Mvono akikumbusha jitihada za baba yake enzi za uhai wake alipohakikisha anasimamia vyema maendeleo yake shuleni.

“Kwa hivyo, matokeo haya ni kwa ajili yake na ninataka baba asherehekee na sisi kutoka huko aliko,” anasema kijana huyo huku akionekana kulengwalengwa na machozi.

Mama yake mzazi, Upendo Komba anasema biashara ndogondogo anazofanya baada ya mumewe kufariki, ziliweza kumsaidia mwanae kupata mafanikio hayo.

“Natamani baba yake angekuwa hapa na sisi leo. Sote wawili tuliamini uwezo wa mtoto wetu. Nilijua anaweza kuwa miongoni mwa kumi bora, ingawa yeye (mwanafunzi) hakuwahi kutarajia,” alisema.

Nilikuwa napika, nataka niwe Askofu

“Nimeokota embe chini ya mpera, nimepata taarifa hizi nikiwa napika na sikuweza hata kula kwa furaha niliyokuwa nayo.”

“Namshukuru Mungu sikutegemea kabisa kuwa namba mbili kitaifa, nafasi hii naichukulia kama zawadi kutoka kwake kuja kwangu,” anasema Denis Kinyange mhitimu wa Nyegezi Seminary ya jijini Mwanza.

Denis amebeba ndoto ya kuwa padri aliyebobea katika taaluma ya udaktari wa upasuaji wa mfumo wa fahamu.

“Nawaomba wazazi wangu wanisaidie kutimiza ndoto yangu ya kuwa daktari pia askofu wa kanisa katoliki. Ninachoiomba familia yangu ni kunisimamia masomo yangu hadi ndoto yangu itimie,” anasema Denis.

Stephen Kanyange ambaye ni baba mzazi wa Denis, alisema mtoto wake kutajwa kuwa mwanafunzi bora wa pili kitaifa ni jambo la kheri kwani hakuna historia ya mtu aliyewahi kushika namba hiyo katika ukoo wao.

Nilikata tamaa, ni Mungu tu

Agatha Mlelwa aliyeshika nafasi ya saba kutoka St Francis anasema alipata matokeo hayo kwa baba yake huku akishindwa kuamini alichosikia. “Ni Mungu tu maana nilikuwa nimeshakata tamaa kwa sababu kila nilipotoka chumba cha mtihani nilikuwa na majonzi kwa kushindwa swali fulani, nikaamua kuacha liwalo na liwe,” anasema Agatha.

Anasema yote kwa yote kumuomba Mungu, kufuata ratiba aliyojiwekea na kujipa muda wa kupumzika kupitia kuimba ni miongoni mwa vitu vilivyochangia kupata matokeo hayo. “Malengo yangu ni kuwa daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa sababu naweza na ninataka kuokoa maisha ya watu,” anasema Agatha.

Wakati Aghata akieleza hayo, Shammah Kiunsi wa shule hiyo hiyo ambaye alishika nafasi ya tisa alilazimika kupiga goti na kumshukuru Mungu juu ya kile kitakachotokea hata kama kitakuwa kibaya.

“Lakini baada ya kuangalia na kuona nimepata ‘A’ katika masomo yangu nilifurahi sana na hasa baada ya kujua kuwa nimekuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kitaifa,” anasema.

Shammah (16) anasema mbali na kusoma, “mimi napenda kupiga gitaa, kinanda na kusikiliza miziki ya taratibu katika muda wa mapumziko lakini pia napenda kusoma vitabu na ninajaribu kuandika.”

“Kuna wakati wa likizo nilikuwa nafanya kazi katika kiwanda cha chakula kwa saa 6 ili nisikae bure nyumbani na sasa hivi nafanya kazi kituo cha watoto kiitwacho Hope for the Future na ninaahidi kidato cha sita nitashika nafasi bora zaidi ya sasa,” anasema mwanafunzi huyo mwenye ndoto za kuwa mchumi mbobezi huku akiwaasa wanafunzi waliobakia shuleni kusoma kwa bidii.

Hajaridhika na matokeo

Wakati wengine wakifurahia matokeo hayo, Lucy Magashi aliyeshika nafasi ya kumi kutoka Huruma Girls ya Dodoma anasema licha ya kutamani kuingia 10 bora lakini alitamani aongoze wengine. Ndoto yake ni kuwa daktari bingwa wa watoto.

Hata hivyo Bernard Magashi ambaye ni baba wa Lucy anasema kama mzazi ni faraja kuona mwanaye anafanya vizuri katika masomo yake kwa sababu ni hazina kwao.

Kwa upande wake, Erick Mutasingwa kutoka Sengerema Seminary aliyeshika nafasi ya tatu alisema jitihada za kujisomea kusikiliza anachofundishwa na kutokata tamaa ndiyo siri ya mafanikio yake kufanya vizuri. Ndoto yake ni kuwa daktari wa upasuaji wa moyo.

Anusurika kifo

Wakati wenzake wakitoa simulizi, Michael Aron (20) aliyehitimu St Agrey Chanji mkoani Rukwa ambaye ni mkazi wilayani Mbozi mkoani Songwe amenusurika kifo baada ya kunywa sumu ya kuua magugu (gramaxone).

Michael alifikia uamuzi huo baada ya kupata daraja la nne badala ya la kwanza ama la pili kama alivyotarajia na sasa amelazwa hospitali ya mkoa wa Songwe (Vwawa).

Alidai kuchukua uamuzi huo baada ya kughadhibishwa na matokeo hayo mabaya.

Matrida Kibona ambaye ni dada wa Michael alisema juzi asubuhi alimuomba simu ili aangalie matokeo na alionyesha kupigwa butwaa kufuatia matokeo aliyoyaona.

“Baada ya kuona amechanganyikiwa nilijaribu kumtia moyo kwa kumsihi asiwaze sana kwani huo hautakuwa mwisho wa ndoto yake kisha niliondoka.”

“Lakini kabla sijafika mbali nilipigiwa simu na majirani nikitakiwa kurudi nyumbani, nilipofika nilipata taarifa kuwa amekimbizwa hospitali,” alisema Matrida.

Matrida alisema siku zote mdogo wake katika maongezi yake alikuwa anatarajia kupata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza ili baadaye atimize ndoto zake za kuwa daktari.

Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya mkoa Songwe, Dk Ahmed Ramadhan alisema wanaendelea kumhudumia mgonjwa huyo na hali yake inaendelea vizuri.

Imeandikwa na Aurea Simtowe, Mosenda Jacob (Dar), Daniel Makala (Sengerema), Mugongo Kaitara (Mwanza) na Stephano Simbeye (Songwe).

Chanzo: mwananchi.co.tz