Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi ya kusikitisha mama na watoto walivyoteketea ndani ya nyumba Iringa

Moto Iringa Kw.jpeg Simulizi ya kusikitisha mama na watoto walivyoteketea ndani ya nyumba Iringa

Thu, 27 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku ya msiba haikuwa rahisi kuzungumza na Skolastika Mgombewa, mama wa watoto wawili waliopoteza maisha baada ya kuteketea kwa moto katika eneo la Mafifi, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Baada ya mazishi yaliyofanyika jana kwenye makaburi wa Ngome, Skolastika amepata nafasi ya kusimulia mkasa wa tukio hilo mpaka kuwapoteza watoto wake.

Mama huyo anatuhumiwa kuwasha mshumaa, kufunga mlango kwa nje, kisha kwenda kunywa pombe, jambo lililosababisha watoto hao kukosa msaada wakati moto ulipoanza kuwaka.

Rehema Sanga (7) na Amos Sanga (5) walifariki dunia baada ya mshumaa waliokuwa wanatumia kushika godoro na kuteketeza nyumba.

Akizungumza na Mwananchi, Skolastika alisema malezi ya watoto wake yalikuwa magumu na kwamba awali walinusurika kufa kwa utapiamlo kabla ya moto uliochukua maisha yao juzi.

“Naumia, nawapenda watoto wangu, mwanzoni waliponea chupuchupu wakati wadogo, ilikuwa wafe kwa utapiamlo, hali ilikuwa mbaya kwa sababu wamekua huku kadi ikisoma alama nyekundu.

“Watoto wangu walipona kwa misaada ya wazungu, hivyo maisha yao mpaka umauti yalikuwa ni misaada ya wazungu,” anasema.

Mpaka sasa Skolastika amefiwa na watoto sita, wanne wakifa kwa magonjwa na wawili kwa ajali ya moto.

Anasimulia kuwa siku ya tukio aliondoka nyumbani asubuhi kwenda kudaka mitumba kwa ajili ya kuuza, kazi ambayo huwa anaifanya.

“Nilidaka nguo tano, nikatembeza, lakini siku hiyo biashara haikuwa nzuri. Kabla sijaondoka nilipika ugali mkubwa wakala asubuhi na nikawawekea wale mchana wakipata njaa,” anasema kwa kunong’oneza baada ya sauti yake kukauka kwa kulia.

Mbali na kudaka mitumba, kazi zake nyingine ni kibarua wa kufua nguo kwenye nyumba za watu, kuokota kuni na kuuza pamoja na kusuka nywele za kawaida kwa bei ya Sh500 au 1,000.

Anasema kuwa alirudi nyumbani saa moja usiku na kuwakuta watoto wake wakiwa salama.

“Niseme tu, kabla sijarudi nyumbani ile jioni, saa kumi nilinunua pombe ya kienyeji ya Sh500 nikanywa, hata saa moja nilipofika nyumbani nilikaa na watoto wangu,” anasema Skolastika.

Nyumba ya Skolastika ipo mlimani, eneo ambalo huwezi kufika kwa usafiri wa aina yoyote.

“Niliondoka tena nyumbani saa tatu usiku, nyumba yangu ina milango miwili wa nyuma na mbele, kwa hiyo mlango wa nyuma ulifungwa kwa ndani na wa mbele nikafunga kwa nje,” anasimulia.

Anasema mlango aliokuwa amefunga kwa ndani ilikuwa inawezekana kufungua kama watoto wangeweza kutoka chumbani ambako ndiko walifia.

“Kule chumbani sikufunga mlango, inawezekana katika kuhangaika watoto walishindwa kuufungua ulikuwa umejibana,” anasema.

Anasema aliporudi saa nne usiku alishangaa kuona watu wamejaa nyumbani kwake huku wengine wakipiga kelele.

“Nilipata bumbuwazi, nilichanganyikiwa jamani watu wakafikiri nimelewa. Nilikunywa saa kumi pombe ya Sh500,” anasema.

Hali ya maisha ya nyumbani

Mtoto wa kwanza wa Skolastika, Sara Sanga anasema ni kawaida kwa familia yao kulala njaa kwa sababu ya ugumu wa maisha.

Sara amebakiwa na wadogo zake wawili wa kike ambao wanafanya kazi za ndani. Anasema kati ya watoto wote, waliosoma zaidi ni wale walioishia darasa la tano. “Kuna wakati tulikuwa tunakwenda na mama kuokota kuni, kufua nguo kwa watu na wakati mwingine tulikosa kazi, tulikunywa uji au kulala njaa.

“Mimi nilifanya kazi za nyumbani kwa watu, baadaye nikapata mwenzangu nimeolewa na sasa nina watoto wawili, mama amepambana kutusadia kadiri ya uwezo wake,” anasema.

Anasema wadogo zake waliofariki walikuwa hawajawahi kusoma darasa lolote, akiwemo wa miaka saba.

“Kweli elimu ni bure, lakini uwezo wa mama ni hela ya kula tu. Hawezi hata kumudu michango na ada shuleni,” anasema.

Skolastika anasema angeweza kuwasomesha watoto wake, lakini hakufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.

“Si kwamba baba yao aliwatelekeza watoto, naye hana uwezo japo tulitengana. Hata nikiomba alikuwa hana ningefanyaje? Pamoja na kuhangaika nilikosa na wakati mwingine niliomba msaada ambao pia sikuwa napata,” anasimulia.

Baadhi ya majirani wamekiri familia hiyo kupitia changamoto za ugumu wa maisha, licha ya kuwa hazisababishi kushindwa kuwa makini kwenye suala la malezi ya watoto.

“Ni kweli watoto wa hii familia hawakuwa wanasoma, lakini angewaacha kwenye usalama kabla ya kuondoka,” anasema Yusufu David, mmoja wa majirani.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Rabi Mgata anakiri familia hiyo kuwa na changamoto za kiuchumi, huku akiishauri jamii kujenga tabia ya kusaidia, hasa mahitaji ya chakula.

Mtaalamu wa saikolojia, Paul John anasema huenda mama huyo alikuwa anatumia pombe kama njia ya kujifariji kutokana na hali ya maisha anayopitia.

“Bado kuna haja ya kusikiliza pande zote mbili kabla ya kuhukumu, pia kuwasaidia wale wanaopitia changamoto ambayo inajulikana. Msaada sio kuwapatia fedha, hata kuwapatia kazi za kufanya,” anasema John.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Issa Juma ameitaka jamii, hasa wazazi na walezi kuwa makini kwa kuhakikisha watoto wao wanakuwa salama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live