Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi wanawake wa Longido waliogeukia mkaa kuikabili njaa

9d194c7977afb2a33033e531f7bb56e7 Simulizi wanawake wa Longido waliogeukia mkaa kuikabili njaa

Fri, 28 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

"Wakati mume wangu anaondoka, aliniachia mbuzi ili niwauze na kununua chakula, lakini walikufa wote kwa kukosa malisho. Tangu aondoke hapa mwezi wa tatu (Machi) hadi sasa (Oktoba) hali ni mbaya, hatuna chakula,"

Ngoje Maso, mkazi wa Kijiji cha Otepesi wilayani Loliondo mkoani Arusha anasimulia madhila yanayowapata kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ngoje, mama wa watoto watatu anaendelea kuwasilisha kinachowasibu, akitamka: "Kwa sasa chakula tunachoona ni muhimu kwetu ni uji, tunalazimika kukoroga uji mchana na jioni kwa sababu hautumii unga mwingi.  Hata ukifanikiwa kupata kilo mbili kwa jirani unaona bora ukoroge uji, uweke na chumvi kwa sababu wenyewe unakuwa mwingi, mara chache tunasonga ugali.

"Wale mbuzi nilioachiwa na mume wangu ili niwauze na kununua chakula, walikosa malisho, wakakosa nguvu na wengine wakaugua. Hata nilipotaka kuwauza, wateja waliwakataa, wakawa wanakufa mmoja mmoja mpaka wakaisha wote.

"Nimeelemewa sasa kutunza hawa watoto, maana kula kwao na mahitaji mengine yakiwamo ya shule ni juu yangu, sijui itakuwaje hali ikiendelea hivi, maana hatuna chakula.

"Mume wangu alilazimika kuondoka hapa kwenda kutafuta malisho baada ya kuona ng`ombe wanazidi kufa, tulikuwa nao wengi lakini wengi wameteketea, kila kukicha tulikuwa tunakuta wamedondoka, wamekufa, wengine wanafia machungani. Ukiamua kuwauza, hakuna wanunuzi, wateja hawawataki, wanasema wamekonda mno."

Familia hiyo ni sehemu ya jamii kubwa ya wananchi wa Loliondo waliokumbwa na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi, wanaume wakilazimika kuziacha familia zao kwenda kutafuta malisho ya mifugo, huku baadhi ya wanawake wakigeukia kuchoma mkaa, shughuli ambayo ni ngeni kushuhudiwa katika jamii ya Kimasai inayosifika kwa ufugaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo.

Nipashe iliyopiga kambi wilayani hapa, imeshuhudia ugumu katika upatikanaji wa maji, chakula na malisho ya wanyama, wananchi wakiiomba serikali na wadau wake kuwanusuru kwa kuwapelekea huduma muhimu.

Katika udadisi wake wilayani Loliondo, Nipashe imebaini kuwa katika familia nyingi za wafugaji, waliobaki nyumbani kipindi hiki cha ukame ni kinamama na watoto wao pamoja na wanaume wachache waliokutwa katika baadhi ya kaya ni waliokula chumvi nyingi, yaani wazee.

WANAWAKE NA MKAA

Sandeki Yaro, mkazi wa Kijiji cha Orubomba wilayani hapa, anasema mume wake aliondoka kwenda kutafuta malisho ya ng`ombe na kumwachia majukumu ya mlezi wa kaya yenye watoto watano.

Anasema baada ya ng`ombe na mbuzi wachache alioachiwa na mume wake kufa kwa kukosa malisho, alianza kuchoma mkaa, malighafi zake zikiwa ni kinyesi cha mbuzi na magogo madogo ya miti.

“Hali ni mbaya sana hapa kama unavyoona, ukame unatisha, inatubidi tutumie akili ya ziada kutafuta namna ya kunusuru familia.

Kwa sasa tumebuni mbinu nyingine ya kutumia magogo madogo ambayo tunaokota msituni kutengeneza mkaa. Tunapoyapata, tunakata vipande vidogo, tunafunika na kinyesi cha mbuzi na tunawasha moto, unakuwa unawaka kidogo kidogo, ndani ya siku tatu tunatoa.

“Kwa kutumia mbinu hii hatuweki magogo mengi, inakuwa ni kidogo tu ambayo tunatoa debe moja au mawili ya mkaa ambalo tunauza kwa Sh. 2,000. Na ukipata hiyo unakwenda kununua unga kilo moja.

“Na hii karibu wanawake wengi wa hapa Longido wamelazimika kufanya hii kazi, kwa sababu wanaume hawapo, wamekwenda kuhangaikia mifugo huko mbali, kuna waswahili eneo la mjini ndio tunategemea wanunue, sisi wenyewe hatutumii mkaa," anasema.

Mama huyo wa watoto watano anasema kazi hiyo ya kutengeneza mkaa ni ngumu kutokana na kuwa na moshi mwingi, akitamka: "Hivi tunavyozungumza (juzi) nina wiki moja sijaifanya kwa sababu niliugua mgongo, nikilala ndio kila kitu kimelala."

PUNJE ZA MAHINDI

Sandeki anasema njia nyingine wanayotumia kujiokoa dhidi ya baa la njaa ni kwenda kutafuta mahali kulipo na mashine za kusaga, mahindi yanayokuwa yamedondoka chini huyaokota na kinachopatikana ndicho wanasaga kwa ajili ya chakula chao.

"Kama hivi ambavyo nimeugua mgongo, ninashindwa kutengeneza mkaa, ninaamka asubuhi kuwahi kwenda kutafuta mashine ya kusaga niokote punje ninayoiona imedondoka. Kuna siku unapata hata nusu kilo au kilo moja, lakini kuna siku nyingine hasa za Jumapili inakuwa ni vigumu kupata.

"Nikishapata hicho kidogo, ninamwomba anayesaga anipatie hata kazi ya kufagia ili anisagie nipate unga kwa kiasi hichohicho cha mahindi nilichookota. Na ukikosa kwenye mashine moja kama hawajadondosha ni mara chache ukienda kwenye mashine nyingine upate kwa sababu kote huko unakuta na wenzio nao wameokota, wengi wamegundua, wanafanya hivyo," anasimulia.

BIASHARA YA MKAA

Katandee Tobiko, mkazi wa Kijiji cha Kimotoro, anasema jitihada zao kukabiliana na baa hilo, wakati mwingine zimekuwa zikikwaza maofisa wa serikali wanaowapoka mkaa.

“Mara nyingi tunapotengeneza huu mkaa huwa tunapeleka katikati ya Mji wa Longido kwa sababu pale kuna waswahili wengi ili wanunue. Tukiwa tumeupanga, unashtukia watu wamekuja na gari lao wanauchukua, wanamiminia kwenye gari wanaondoka wa wanaturushia viroba vitupu, hatujui wanatoka wapi ila gari lina namba za serikali na huwa wanatuambia hatutakiwi kuuza mkaa.

"Yaani pamoja na hali mbaya tuliyonayo, hawatuonei huruma, wanatubebea mkaa bila huruma, tunarudi nyumbani mikono mitupu na watoto wetu wanalala njaa," anawasilisha.

MAHINDI YA SERIKALI

Kiongozi wa Mila Wilaya ya Longido, Mutel Laizer anasema hali ya njaa ni mbaya katika vijiji vingi vilivyopo kwenye wilaya hiyo iliyosababishwa na ukame.

“Familia nyingi zinalia njaa, hazina chakula. Tumeshuhudia serikali ikileta chakula kwa bei nafuu katika wilaya hii lakini kinauzwa kwa bei kubwa ambayo wengi wanashindwa kumudu. Hata kinapoletwa, wanawaambia wanunue kuanzia gunia moja, wengi hawana uwezo huo.

“Mimi kama kiongozi wa mila, nimeliongelea sana hili lakini haijasaidia, wananchi wana njaa, wanashindwa kumudu bei ya chakula, lakini hata kile kinacholetwa na serikali nacho kinauzwa kwa bei kubwa, tena kuanzia gunia. Je, hapa kuna nia ya kuwasaidia kweli?.

"Tunachoona ni kwamba serikali inaleta chakula kwa ajili ya kupunguza makali ya wananchi, lakini wanaonufaika watu wenye uwezo, hasa wafanyabiashara, kwa sababu wao wana uwezo wa kununua gunia au zaidi na mwisho wa siku wao watakiuza kwa bei kubwa kwenye maduka yao. Tunaomba serikali iangalie hili," Laizer anasema.

Anabainisha kuwa debe la mahindi kwa sasa linauzwa na wafanyabiashara wa kawaida kwenye maduka yao kwa Sh. 22,000.

“Kwa hiyo kila mahali unakogeukia unakuta kugumu. Kwa wafanyabiashara bei iko juu zaidi, ukija kwa serikali ambako bei yao ni angalau kidogo, nao wameweka masharti magumu upatikanaji wa chakula chenyewe. Wanamwambia mwananchi ambaye hata uwezo wake wa kununua kilo moja ni mgumu, eti anunue gunia, hii ni hatari.

"Tunachoomba kama ikiwezekana, wapunguze zaidi bei hii ya chakula na kwa wale wasio na uwezo kabisa wawaangalie namna ya kuwasaidia hata wakiwapatia chakula kidogo itasaidia," anawasilisha.

Ni hoja inayoungwa mkono na Marya Oreteiti, mkazi wa Kijiji cha Longaiki, anayesema familia nyingi zinashindwa kumudu kununua chakula kinachouzwa na serikali.

“Sisi chakula cha serikali hatujakinusa hata kidogo. Ukienda kule wanakuambia eti ununue gunia moja. Unaona bora uende ukanunue kule kwa wafanyabiashara wa kawaida ambao wanapima hata kidogo ili familia ipate kula," anasema.

*ITAENDELEA....

Chanzo: www.tanzaniaweb.live