Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi mtoto wa miaka 10 alivyobakwa na jirani

Ubakajiiii Simulizi mtoto wa miaka 10 alivyobakwa na jirani

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: mwanachidigital

Ni unyama, ndiyo unavyoweza kutafsiri alichofanyiwa mtoto mwenye miaka 10, mwanafunzi wa darasa la saba.

Amebakwa mara nne kwa nyakati tofauti na jirani yao, mwanamume mwenye miaka 40.

Mwanafunzi huyo, mkazi wa Kijiji cha Sanganga, Kata ya Pemba wilayani Tarime, anadaiwa kutendewa ukatili huo na Kassim Mwita. Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda ya Tarime/Rorya, Mark Njera.

"Tayari upelelezi umekalika na mtuhumiwa tutamfikisha mahakamani," amesema.

Mkasa huo umeibuliwa na wataalamu wa afya walipotoa elimu ya afya ya uzazi na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) chini ya mradi wa kuwezesha vijana unatokelezwa Wilaya ya Tarime mkoani Mara na Shirika la Children’s Dignity Forum (CDF).

Baada ya kubaini uwepo wa tukio hilo,tulifunga safari ya zaidi ya kilomita 20 kutokea kituo cha mabasi Tarime mjini hadi Kata ya Pemba anakoishi mtoto na mtuhumiwa.

Baada ya kupokewa na wazazi wake, walitueleza mkasa mzima na tulipata nafasi ya kufanya mahojiano na mtoto huyo.

Simulizi ya mtoto

Mtoto huyo ambaye muda wote alikuwa akitokwa machozi, alidai kuwa si mke wa Kassim, shuleni wamekuwa wakimuita hivyo, halipendi jina hilo.

Haikuwa rahisi, akiwa amezungukwa na wadogo zake alikuwa akitokwa mchozi.

Baadaye amesimulia;“Desemba 26, 2023 nilikwenda kuchota maji kwa Kassim, akaniita nikaenda. Nilimuuliza anachosema, alinielekeza nipeleke maji ndipo nirudi upesi.

Nilipeleka maji na kurudi kwake, akanikaribisha ndani, kufunga mlango na kuingia chumbani. Baada ya muda mfupi alitoka ameshika panga na kuniambia ole wako upige kelele nitakuchinja.

Niliogopa, akaniambia vua nguo zote, (analia huku akifuta machozi) akaniwekea uume sehemu zangu za siri, niliumia.

Desemba 29, 2023 nilitumwa tena maji kwake, wakati nachota aliniita akiwa anakatia majani mifugo yake, akanishika mkono.

Alinipeleka kwenye nyumba ambayo haikuisha ujenzi, akanilaza chini na kuniingilia baada ya kumaliza aliniambia vaa nguo ondoka na ole wako umwambie mtu nakuua.

Desemba 30, 2023 nilitumwa tena maji nyumbani kwake, mke wake hakuwapo wala watoto, alinipeleka ndani akanivua nguo na kuniingilia.

Desemba 31, 2023 nilikwenda tena kuchota maji, akaniita, nilimwambia nasikia uchungu aliniambia hatoniingiza tena. Alinichukua na kunipeleka ndani, aliniingiza vidole sehemu za siri.

Sikusema kwa mama wala baba, niliogopa nilijua mama atanichapa japokuwa nilikuwa nahisi maumivu makali.

Ushuhuda

Nduguye wa kiume anayesoma darasa la sita anasimulia alivyoshuhudia tukio hilo, lakini hakujua kilichokuwa kinaendelea.

Mama alinituma nikamuite (dada yake aliyebakwa) nikamkuta Kassim amepiga goti na dada kalala chini nikamwambia mama anakuita.

Alivyotoka akaenda dukani, sikumwambia mama kwa sababu sikuwa najua.

Alivyogundulika

Ruth Masanje, mama mdogo wa mtoto huyo anayeishi naye, amesema baada ya kumuona alibaini hayuko sawa kwa namna alivyokuwa akitembea.

"Mtoto amekuja ananyanyua kifua na makalio juu, nilihisi hiyo si kawaida yake, kuna jambo haliko sawa,” amesema.

Baadaye amesema mwanaye huyo alimuomba dawa aina ya rangi mbili akisema ana maumivu ya kichwa.

“Nilimwambia nenda kachukue kwa baba yako dukani hakutaka, bali alianza kutokwa machozi. Nilimbembeleza aniambie tatizo, aliendelea kulia,” amesema.

“Nilimpigia simu baba yake, alipokuja bado hakutaka kusema. Baba yake aliniambia nenda kamkague nilimchukua na kwenda kumuangalia, kweli nilikuta uke umepanuka, nilishtuka na mwili ulianza kutetemeka,” amesema.

Amesema aliwaita majirani kushuhudia tukio hilo. Mtoto alipoulizwa alikataa kuzungumza, bali aliendelea kulia.

Amesema baba yake alichukua fimbo na kutishia kumchapa endapo hatazungumza, hivyo alimuomba baba yake mdogo asimuadhibu, kwani yupo tayari kueleza ukweli.

Amesema alimuita mwenyekiti wa kijiji aliyeenda kumhoji mtuhumiwa.

Ruth amesema wananchi walijitokeza wakitaka kumchukulia hatua kali mtuhumiwa, lakini polisi walifika na kumchukua mtuhumiwa na mtoto aliyepelekwa hospitali kwa uchunguzi.

Amesema wataalamu walimpatia mtoto huyo dawa kumkinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Ruth ameliomba Shirika la CDF kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matukio ya ukatili, akiiomba Serikali itende haki kwa mwanaye.

Mtuhumiwa matatani

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Mark Njera amesema mtuhumiwa alitoroka baada ya kutenda kosa hilo, ndipo jeshi hilo lilipoanza msako na kumkamata wiki iliyopita.

"Mtuhumiwa tumemuweka ndani kwa muda wote kwa sababu mbalimbali zikiwamo za usalama, yule mtoto aliharibiwa sana, hivyo wananchi walitaka kumuua na hata siku alipokamatwa wananchi walifika kituoni wakitaka kumuadhibu," amesema Kamanda Njera.

Amesema upelelezi wa tukio hilo umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu makosa yanayomkabili.

Mwenyekiti wa kijiji, Leonard Karoche amesema aliwazuia wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuhakikisha vyombo vya dola vinamtia nguvuni mhusika.

"Sikufurahishwa na tukio hili la kinyama, nilisikia matukio mengine ambayo amekuwa akiyafanya Kassim, lakini hayakuripotiwa hili ndilo tukio nililiona, niwaombe wazazi wahakikishe wanasimamia usalama wa watoto wao. Haya mashirika ya kiraia kama CDF na mengine waendelee kutoa elimu kwa wananchi," amesema.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Sirari wilayani Tarime, Dk Anna Mruga amesema baada ya mtoto huyo kufanyiwa uchunguzi amebainika kuwa na shahawa ndani ya uke na damu.

"Tulimpima mtoto na kudhibitisha amebakwa,” amesema.

Mkurugenzi wa Shirika la CDF, Koshuma Mtengeti amesema kuibuliwa kwa tukio hilo ni kiashiria cha wananchi kupata uelewa wa masuala ya ukatili unaofanyika kwa watoto.

"Tutaendelea kutoa elimu kuhakikisha matukio haya hayakaliwi kimya, elimu ya uzazi, ukatili na udhibiti wa VVU kwenye jamii utakuwa endelevu," amesema.

Chanzo: mwanachidigital