Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi mtoto aliyedondoka mtini

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Japokuwa sura inaonekana kujaa tabasamu, lakini Moses Gabriel (14), mwanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Samora Machel mjini Mbeya hawezi kuinuka kitandani wala kunyanyua miguu baada ya kuvunjika uti wa mgongo.

Moses alivunjika uti wa mgongo miezi minane iliyopita baada ya kuanguka kutoka juu ya mti alipotumwa na mwalimu wake kukata fimbo za kuwachapia wanafunzi.

Tangu wakati huo, mwanafunzi huyo hajaweza kwenda tena shuleni, anaendelea kuugulia maumivu makali akiwa kitandani huku mama yake mzazi, Swaumu Ramadhani akipambana kumuuguza.

Simulizi ya Moses kwa Mwananchi, nyumbani kwao Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam inaanzia asubuhi ya Aprili 25, alipowasili shuleni na kuingia darasani.

Anasema siku hiyo mwalimu wa Hisabati aliingia darasani akiwa amekasirika baada ya wanafunzi kufeli somo hilo.

Moses anasema, baada ya kuingia, mwalimu aliwauliza kwa nini wamefeli na aliwasimamisha wanafunzi wawili kwenda kutafuta fimbo ambazo angezitumia kuwaadhibu.

“Alinichagua mimi na mwenzangu, tukatoka nje kwenda kutafuta fimbo, chini hazikuwa zikipatikana ikabidi nipande juu ya mti kuzivunja,” anasimulia. Alikata fimbo akamaliza, lakini wakati anataka kushuka aliteleza na kuanguka

“Nilitua (chini) kwa kichwa, ikafuata shingo, mgongo na wakati najiokoa nilitumia mikono nayo ikapinda na kuvunjika.”

Kijana huyo anasema mwanafunzi mwenzake baada ya kuona ajali hiyo ilibidi akimbie hadi kwa mwalimu kumweleza.

Anasema, “Walimu walikuja wakachukua gari la mkuu wa shule na kunipeleka hospitali, kusema kweli niliumia sana na hali yangu haikuwa nzuri.”

Huku akiwa amejilaza kwenye godoro lililowekwa sakafuni sebuleni nyumbani kwao, Moses anasema akiwa hospitali, baadaye aliingizwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi. “Walinipima mikono wakaona imevunjika, pia shingo nayo ikawa hivyohivyo, walinivisha vifaa vya kunisaidia nikalazwa Hospitali ya Rufaa Mbeya.”

Wakati akisimulia, umeme ulikuwa umekatika, hivyo alikuwa akilalamika joto kali ambalo lilikuwa linampa wakati mgumu kwa sababu hakukuwa na njia nyingine ya kulipoza.

Swaumu, mama yakeMoses anasema siku ya tukio alishtushwa na simu aliyopigiwa na walimu akiambiwa kuwa mwanaye amepata ajali baada ya kuanguka kwenye mti wakati akikata fimbo. “Nilishtuka kweli, nikawauliza hali yake ikoje wakasema ameumia sana hivyo natakiwa niwahi jijini Mbeya,” anasema.

Anasema ilibidi aanze mchakato wa kutafuta nauli na siku ya tatu alifanikiwa kusafiri.

“Kule Mbeya ni kwa baba yake mwanangu, hivyo siku ya tatu nilifika usiku sana, sikuweza kwenda hospitali kwa wakati huo, nililala hadi asubuhi nikajihimu kwenda kumuona.”

Anasema alimkuta akiwa na hali mbaya pamoja na maumivu makali na alipomuuliza kama anamkumbuka, alijibu, “Wewe ni mama, basi nikajua hajapoteza kumbukumbu zake nikashukuru Mungu.”

Swaumu anasema, “(madaktari) hawakumpima (Moses) mgongo, ila maeneo mengine kama mkono na shingo walikuwa wameshampa msaada na wakanieleza wazi kwamba natakiwa kupewa rufaa kuja Muhimbili.”

Alianza kushughulikia rufaa ambayo anasema ilichelewa kutolewa, “Tangu waniambie rufaa zilipita siku tatu ikabidi niwaulize kama ni kweli mtoto anahitaji au hahitaji hiyo rufaa, basi wakanipatia nikaanza safari ya kumleta huku Dar es Salaam.”

Kwa sasa mwanafunzi huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kuhusu uongozi wa shule hiyo kusaidia gharama za matibabu za mwanaye, Swaumu anasema awali walimu walikuwa wakipokea simu zake na kumpa ushirikiano, lakini baadaye wakaacha.

Baadaye mkuu wa shule alimwambia wameshatoa huduma ya kwanza wanayopaswa kuifanya, lakini si mwendelezo wa matibabu. Hata hivyo, juhudi za kuzungumza na uongozi wa shule hiyo jana zilishindikana baada ya kukataa mpaka utakapopata ruhusa ya mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Mbeya, James Kasusura ambaye jana hakupatikana kuzungumzia ruhusa hiyo.

Maombi ya Moses

Wakati akiendelea na matibabu, Moses anaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kumpeleka nje ya nchi kutibiwa kama ilivyotokea kwa watoto wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha waliopata ajali Mei 6, 2017.

“Wale watoto walienda wakiwa kama mimi, lakini walirudi wanatembea, naomba msaada na mimi nipelekwe huko, natamani kusoma nitimize ndoto zangu ili nije kumsaidia mama yangu,” anasema Moses.



Chanzo: mwananchi.co.tz