Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi chungu maisha ya Mariamu kwa miaka 20

53067 Pic+mariam

Fri, 19 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jumatano ya Aprili 17 inaweza kuwa siku muhimu kwa Mariam Rajab, msichana aliyeuguza kidonda mgongoni tangu Agosti, 2018.

Siku hiyo ndipo alipotua jijini Dar es Salaam akitokea Singida kwa ajili ya kuanza matibabu mapya ya kidonda hicho katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya juhudi za awali kijijini kwao kuonekana kutofanikiwa.

“Sasa nina matumaini ya kupona baada ya Serikali kujitoa kugharimia matibabu yangu na gharama zote,” alisema Mariam akiwa wodi ya Kibasili jana.

Serikali ilichukua hatua ya kumsafirisha kutoka Singida baada ya video inayomuonyesha akiomba msaada wa matibabu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa siku kadhaa.

Historia ya tatizo hilo ni ndefu. Chanzo cha kidonda hicho ni jeraha la moto alilolipata akiwa na umri wa miaka mitano, alisema Mariam.

Binti huyo ambaye sasa ana miaka 25, alisema akiwa na miaka mitano wakati anaota moto nyumbani kwao, nguo yake ilidondokea motoni aliiokota na kuikung’uta.

Baada ya kuamini kuwa moto umezimika, aliichukua na kuitupia mgongoni, kumbe ilikuwa bado na moto ambao uliunguza mgongo wake, anasema dada yake Mariam, Tatu Rajab aliyeambatana naye kwa ajili ya kumuuguza.

Alitibiwa kidonda cha moto na kikapona huku kikiacha jeraha ambalo limebadili maisha yake na kumfanya kuwa mtu mwenye maumivu siku zote.

Takribani miaka 20 baada ya tukio hilo, ulitokea uvimbe kwenye jereha na hatimaye ukapasuka na kutengeneza kidonda.

Tatu alieleza kuwa walihangaika kutibu kidonda hicho kwenye hospitali ya mkoa na hatimaye akafanyiwa upasuaji.

“Upasuaji ule ulifanyika kwa kukata nyama kwenye paja na kwenda kuziba kidonda, kwa wakati ule ulisaidia maana alisema amepona.

“Nakumbuka hiyo ilikuwa mwaka 2015. Tulirudi nyumbani na kuendelea na maisha akionekana wazi afya yake ikiwa imerejea,” alisema Tatu.

Furaha ya familia hiyo ilipotea Agosti mwaka jana baada ya kidonda hicho kufumuka upya na safari hii kikionekana kuongezeka ukubwa.

Mariam alikwenda tena hospitali na huko matibabu aliyopewa yalikuwa ya kukisafisha kidonda hicho kwa gharama ya Sh5,000 kwa siku.

“Sikuwa na uwezo wa kutoa hiyo hela kila siku, nikaomba rafiki zangu wakanisaidia fedha nikanunua dawa, nikawa naitumia kujisafisha mwenyewe nyumbani kwa kuomba msaada wa ndugu zangu,” alisema Mariam.

“Baada ya kujisafisha kuna dawa nyingine za vidonge nilikuwa nasaga na kuziweka kwenye kidonda.”

Kwa mujibu wa Tatu, dawa hiyo ni fragile na walianza kuitumia baada ya kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya aliyewaeleza kuwa inasaidia kuua bakteria.

Matumaini ya Mariam kupata ahueni yanajengwa na jinsi huduma ilivyoanza baada ya kuwasili Muhimbili.

“Tulichokifanya ni kumsafisha na kuchukua vipimo kuangalia hii ni aina gani ya kidonda maana tumeshakiona kuwa si cha kawaida,” alisema Dk Ibrahim Mkoma, mkuu wa kitengo cha upasuaji na daktari bingwa wa nyanja hiyo.

Alisema kwa uzoefu wake, vidonda vinavyotokea kwenye jeraha mara nyingi huwa vina uhusiano na saratani.

“Siwezi kusema hii ni nini hadi tupate majibu, ila kwa uzoefu vidonda vya namna hii vina uhusiano na saratani. Tukishapata majibu ndiyo tutajua ni namna gani tunatibu kutokana na hali ya ugonjwa ilipofikia,” alisema daktari huyo.

“Endapo itakuwa saratani na haijasambaa sehemu nyingine zaidi ya kwenye kidonda, itakuwa rahisi kuondoa na kuweka ngozi nyingine.”



Chanzo: mwananchi.co.tz