Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simanzi, watoto watatu wa familia moja wafa maji Dar

88864 Vifo+pic Simanzi, watoto watatu wa familia moja wafa maji Dar

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna ajuaye siku wala saa ambayo ataondoka duniani. Kifo kimefanywa kuwa fumbo kubwa la imani.

Baada ya kuondoka nyumbani wakiwa na furaha na kwenda ufukweni kubarizi, hawakujua kama ndugu zao Khalfan Said (17), Jalila Said (15) na Rummani Said (14) watafikwa na umauti.

Watoto hao wa familia moja walikufa kwa kuzama baharini juzi wakiwa kwenye Ufukwe wa Bamba, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Baba mzazi wa watoto hao, Said Saleh Omar akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwake eneo la Tandika Majaribio jijini Dar es Salaam alisema siku ya tukio hilo watoto wake walikwenda ufukweni kuburudika na kujipumzisha jambo ambalo wamekuwa wakilifanya mara kwa mara, lakini juzi walikutwa na umauti.

Akiwazungumzia watoto hao alisema Khalfan alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Istiqama ya Pemba, Jalila alikuwa akisoma Tandika Sekondari na wote walikuwa wakitarajia kuingia kidato cha pili mwakani, huku Rummani akiwa anasoma Shule ya Msingi Tandika na alikuwa anatarajiwa kuingia darasa la saba mwakani.

Alisema pia katika ajali hiyo wamempoteza mtoto mwingine wa ndugu yao waliyemtaja kwa jina la Mariam Ramadhani mwenye umri wa miaka 14.

“Ni ajali kama nyingine sina wa kumlaumu, kila mtu ataondoka kwa namna aliyopangiwa na Mwenyezi Mungu, hivyo nashukuru kwa yote yaliyotokea na nimekubaliana na hili,” alisema huku akilengwa na machozi.

Baba huyo wa watoto tisa, licha ya kupata pigo hilo, alisema hana budi kumshukuru Mungu kwa kila jambo.

“Lakini wameniachia pengo kubwa katika familia, japo nilikuwa bado sijajua walikuwa na ndoto gani za baadaye kutokana na umri wao. Mwenzao Mariam alikuwa akisoma Shule ya Msingi Chanjamjawiri Pemba na alikuwa akiingia darasa la saba mwakani, alikuja likizo,” alisema.

Akisimulia tukio lilivyotokea, mjomba wa watoto hao, Ansar Mohammed ambaye pia ni kaka yake marehemu Mariam alisema kutokana na ukubwa wa familia hiyo, siku hiyo waliamua kwenda ufukweni kwa daladala na wengine walitumia magari matatu ya nyumbani. “Tulikuwa zaidi ya 40 na tulifika katika ufukwe huo kama saa saba mchana. Tulicheza, tukala na baadaye tuliwaingiza watoto wadogo katika maji waweze kufurahi.”

“Baada ya watoto wadogo kutoka waliingia hawa wakubwa ambao miongoni mwao ni marehemu na tuliwafundisha kuogelea katika maji ya kawaida kabisa na baadaye tuliwaambia wakae nje ili na sisi tuogelee,” alisema Ansar.

Alisema wakati wao wanaingia kuogelea, mabinti hao na wenzao walikuwa wakicheza mpira eneo lenye maji madogo na hivyo hawakuwa na wasiwasi.

“Sisi tuliogelea hadi kwenye kina kirefu zaidi, baada ya muda kupita tulianza kusikia kama sauti za kuita ‘Mjomba Ansar’ Kaka Ansar’ tusaidie.”

“Wakati kelele hizo zikisikika, kumbe tayari maji ya bahari ambayo ilikuwa imehama kwa wakati huo, yakawa yamerudi kwa kasi bila wao kujua na kuwakuta pale walipo yakawazidi nguvu. Kuna ndugu yetu mwingine anaitwa Soud yeye muda huo alikuwa akiogelea kurejea nchi kavu sisi tulikuwa bado tuko kwenye kina kirefu, alivyosikia hivyo alifanya haraka kwenda kuwasaidia, lakini maji yalizidi kuongezeka na alipowafikia, naye pumzi ikawa inamuishia,” alisimulia mjomba huyo ambaye anasema baada ya watoto kumuona, wote walimng’ang’ania wakazidiwa wote wakawa kama wanazama.

“Wakati hayo yakiendelea sisi tulikuwa tunakaribia na tulipofika tukapiga kelele kuomba msaada, walikuja vijana wengine wawili wakatusaidia, lakini tayari hali ilikuwa mbaya kwa mabinti hawa watatu,” alisema Ansar.

Alisema wakati hayo yakiendelea, Khalfan alikuwa nchi kavu lakini kelele za kuomba msaada zilimfanya arudi majini kuwasaidia.

“Bila kufahamu kuwa kifo kilikuwa kinamuita, baada ya kuwatoa mabinti hao katika maji walipewa huduma ya kwanza ya kuwatapisha maji na taratibu za kuwapeleka hospitali zikafanyika haraka.

“Lakini tulipofika hospitali tuliambiwa tayari wameshafariki ila kwa wakati huo, niligundua Khalfan haonekani, nilipopiga simu nyumbani nikaambiwa hajafika, nikajua tumemuacha kule lakini ilipofika saa saba usiku, tulipigiwa simu na wahusika wa Bamba Beach kutuambia kuwa kuna mwili wameuona wa mtoto wa kiume, tukawapigia simu ndugu zetu wanaoishi karibu na eneo hilo wakathibitisha kuwa mwili ni wa Khalfan.” alisimulia.

Miili ya watoto hao ilizikwa jana katika makaburi ya Wailes Temeke Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Amon Kakwale alithibitisha kupokea taarifa za ajali akisema kuwa ilitokea kwenye ufukwe ya Bamba.

Chanzo: mwananchi.co.tz