Wafugaji wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuwaruhusu waingize mifugo kwenye hifadhi za Taifa zilizopo jirani ili kunusuru mifugo yao inayokufa kutokana na kukosa malisho na maji.
Wametoa ombi hilo ikiwa taatifa zinabainisha kuwa mifugo 62,593 katika vijiji vya wilaya ya Simanjiro imekufa ndani ya mwezi mmoja kutokana na ukame unaosababisha kukosa malisho na maji.
SOMA: Ukame waua mifugo 62,500 Simanjiro
Wakizungumza Januari 15, 2022 baada ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega kutembelea maeneo ya wilaya hiyo ambayo yameathiriwa na ukame, wamesema Serikali ikiruhusu itasaidia kuepusha janga hilo linaloendelea.
Mmoja wa wafugaji hao, Isaya Mollel amesema mifugo mingi imekufa na kusababishia umaskini kwa wafugaji.
Ameiomba Serikali iwaruhusu waingize mifugo pembezoni mwa hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero.
Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Mardadi amesema wafugaji wanapitia wakati mgumu ambapo kwa sasa hata bei ya mifugo imeshuka kutokana na mifugo mingi kukonda.
"Hivi sasa huwezi kuuza hata ng'ombe mmoja kwa Sh200, 000 kutokana na kukonda tunaiomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma kwani hali ni mbaya kwetu wafugaji," amesema Mardadi.
Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri Ulega amesema ombi hilo atalifikisha kwenye mamlaka husika.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega akiwanywesha ng'ombe maji wakati akikagua mifugo iliyokufa kutokana na ukame kwenye kata ya Orkesumet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara Januari 15, 2022. Picha na Joseph Lyimo
"Baada ya kusikia kuwa kuna mifugo imekufa ikabidi kuja kuwapa pole, nawaahidi kuzungumza na viongozi wenzangu wa Serikali juu ya tatizo hilo," amesema Ulega.
Awali, ofisa mifugo na uvuvi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Dk Swalehe Masaza alisema mifugo 62,593 ya eneo hilo imekufa kwa ukame ndani ya mwezi mmoja.
Dk Masaza amesema wilaya hiyo ina ng'ombe 450,187 mbuzi 418,653 kondoo 237,217 punda 22,217 ngamia 55 nguruwe 896 kuku 94,429 na mbwa 7,678.