Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sikukuu za mwisho wa mwaka zilivyowalaza wasafiri stendi

35175 Pic+sikukuu Sikukuu za mwisho wa mwaka zilivyowalaza wasafiri stendi

Tue, 8 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Imekuwa ni kawaida kwa wenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro hususan wachaga kuwaona kila mwisho wa mwaka wakisafiri kwenda mkoani humo kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea Krismasi na mwaka mpya.

Hata hivyo licha ya jambo hilo kusababisha shida kidogo katika usafiri kutokana na ongezeko la abiria, lakini halijawahi kuwa kero kubwa kama ilivyoshuhudiwa mwaka huu.

Katika sikukuu za mwisho wa mwaka 2018 kumekuwa na tofauti baada ya shida ya usafiri kuwa wimbo ulioimbwa karibu kila mkoa huku Kilimanjaro kukionekana kuwa na hali mbaya zaidi.

Idadi kubwa ya watu kutoka nje ya Kilimanjaro iliingia mkoani humo kwa ajili ya mapumziko ya Krismasi na mwaka mpya na kusababisha msongamano mkubwa wa watu na magari tofauti na miaka mingine.

Waziri alanguliwa Ubungo

Kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakisafiri kwenda maeneo mbalimbali kufurika katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo, Dar es Salaam, ilisababisha baadhi ya abiria kukosa usafiri na baada ya hali kuwa tete mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Nchikavu na Majini (Sumatra) ilitoa vibali kwa mabasi zaidi ya 200 ili kukabiliana na adha ya usafiri katika kituo hicho.

Kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 22 mwaka jana, upatikanaji wa usafiri katika kituo hicho cha Ubungo ulikua mgumu na kuibua vitendo vya utapeli na wizi kwa wasafiri waliokuwa wakienda mikoani.

Hali hiyo ilisababisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kufika kituoni hapo na kushuhudia vitendo vya ulanguzi wa tiketi uliokua ukifanywa na baadhi ya madalali ambapo na yeye aliingia katika orodha ya waliolanguliwa.

Mbali na Waziri huyo kulanguliwa tiketi, zaidi ya abiria 20 walikwama Ubungo kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kutapeliwa.

Akisimulia jinsi alivyotapeliwa, Waziri Kamwelwe alisema kwamba alifika kituoni hapo saa 11 alfajiri akiwa na begi lake kama wafanyavyo wasafiri wengine na kupokewa na kijana aliyemweleza kuwa nauli ni Sh35,000.

“Katika ukaguzi nilioufanya kituoni hapo, nimebaini wasafiri kulipishwa nauli tofauti na hii ni kutokana na kuwepo kwa madalali nje ya kituo.

“Ili kukomesha vitendo hivi nitapeleka mapendekezo bungeni la kuanzishwa kwa mfumo wa tiketi za kieletroniki zitakazosaidia kuepusha ulanguzi,” alisema Waziri Kamwelwe.

Hali ilivyokuwa Moshi

Mwananchi ilipiga kambi katika Stendi ya Mabasi Mjini Moshi na kushuhudia msongamano mkubwa wa abiria katika stendi hiyo huku idadi ya mabasi yanayotoa huduma hiyo nayo ikionekana kuwa ni ndogo hali ambayo inaaminika kuwa sababu ya kupanda kwa nauli.

Sio mikoani pekee bali hata kwa wasafiri waliokuwa wakisafiri kutoka wilaya moja kwenda nyingine ndani ya mkoa huo nao walikumbwa na adha ya usafiri kutokana na ongezeko la watu na kusababisha magari kuwa machache hali iliyofanya wasafiri wakae stendi kwa zaidi ya saa nne.

Licha ya kukaa stendi kwa muda mrefu, wakisubiria usafiri kuelekea wilayani humo, nauli nazo pia zilipanda kutoka Sh3,000 hadi Sh5,000.

Laura Shayo, ambaye alikua akisafiri kwenda Tarakea, alisema alikaa stendi kwa zaidi ya saa nne akisubiri usafiri bila mafanikio.

Naye Agustine Kimario, ambaye pia ni miongoni mwa abiria waliokuwa wakienda wilayani humo kutoka Moshi, alieleza kushangazwa kwa kupanda ghafla kwa nauli na kusema jambo hilo linawaumiza wananchi ambao kipato chao ni cha chini.

“Nimekuja hapa na bajeti ya Sh3,000 naelekea Huruma Hospitali kumuona mgonjwa, sasa cha kushangaza nimepanda gari naambiwa kama sina Sh5,000 nishuke...huu ni unyanyasaji,” alisema Kimario.

Foleni katika mji wa Moshi

Mbali na nauli kupanda, wakazi wa mji wa Moshi, walieleza kukerwa na msongamano wa magari katikati ya mji huo na kusababisha watu kukaa barabarani kwa muda mrefu kutokana na foleni ya magari.

Mary Shayo, mkazi wa mjini humo alielezea kukerwa na msongamano mkubwa wa watu na magari katika barabara ya Mbuyuni na barabara za katikati ya mji hali iliyosababisha achelewe katika shughuli zake.

“Nimetoka sokoni kununua mahitaji ya kwa ajili ya sikukuu, lakini nimekumbana na msongamano wa watu na magari njia nzima, hata kama una usafiri binafsi unaweza kusimama barabarani kwa zaidi ya saa mbili,” alisema Mary.

Dereva wa daladala inayofanya safari zake kati ya Kiboroloni na Moshi mjini, Hashimu Issah alisema msongamano huo wa magari umesababisha asimame barabarani kwa zaidi ya saa moja jambo ambalo halijawahi kutokea.

Baada ya Desemba 25

Baada ya Desemba 25, mwaka jana mabasi yalionekana kuwa mengi katika Stendi Kuu ya Mabasi Mjini Moshi na kusababisha yakose abiria yalipokuwa yakirudi Dar es Salaam hali iliyoyalazimu kushusha nauli kutoka Sh32,800 hadi kati ya Sh10,000 na Sh15,000.

Mmoja wa madereva wa magari yaendayo Dar es Salaam, Omari Hamza alieleza kuwepo na changamoto kubwa ya upatikanaji wa abiria waliokuwa wakirudi jijini humo na kufanya baadhi ya magari yarudi bila abiria.

“Sasa tunatafuta abiria kwa shida mno, imebidi tushushe nauli lakini hali ni ile ile...nahangaika tangu asubuhi ili nipate angalau abiria wa kurudi nao lakini hakuna kabisa,” alisema Hamza alipozungumza na Mwananchi Desemba 26 mwaka jana.

Hata hivyo baada ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya licha ya Sumatra kuwaonya wamiliki wa vyombo vya usafiri juu ya kupandisha nauli, bei ya tiketi katika stendi hiyo ilipanda na kuibua malalamiko kwa wasafiri.

Siku moja kabla ya kuamkia mwaka mpya 2019, kulishuhudiwa msongamano mkubwa wa watu waliokuwa wakisaka usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali hususani Dar es Salaam lakini wengi walikwama kutokana na nauli kupanda ghafla.

Wasafiri hao walikua wakitozwa kati ya Sh35,000 hadi Sh40,000 kwa mabasi yaliyokuwa yakienda Dar es Salaam badala ya kati ya Sh25,000 na Sh32,800.

Ashura Jumanne alisema: “Juzi nimelala hapa stendi ili niwahi magari saa 11.00 alfajiri lakini cha kushangaza mabasi yote yakija yamejaa si makubwa wala madogo, mie ni mgonjwa na kesho natakiwa niwe Muhimbili lakini usafiri hakuna.”

Akizungumzia hali hiyo, Gaudensia Tarimo alisema mbali na adha ya kulala stendi usiku walikosa mahitaji muhimu baada ya maduka kufungwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz