Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku tatu zaongezwa kuwasaka waliofukiwa na kifusi mgodini

Thu, 19 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Singida. Siku tatu zimeongezwa  kuwatafuta wachimbaji wadogo wawili wa madini waliofukiwa na kifusi wakati wakichimba dhahabu katika mgodi wa Sekenke mkoani hapa.

Wachimbaji hao walifukiwa na kifusi tangu Julai 6, 2018 na hadi leo Julai 19, 2018 wamefikisha siku 13.

Mgodi huo unaomilikiwa na Sekenke One Mining Cooperative Society Ltd upo Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Waliofukiwa na kifusi hicho katika shimo namba 49 C  ni,  Mwita Wambura (43) na  Yasin Ngumi (30) wakazi wa mkoani Mara.

Akizungumza na MCL Digital leo, kamishna wa madini kanda ya kati,  Sosthenes Massola amesema  baada ya siku hizo tatu kumalizika, wataketi na kutafakari hatua zaidi za kuchukua.

Amesema shughuli hiyo inafanyika mchana na usiku kwa kuzingatia usalama wa waokoaji ili kuepuka kutokea maafa zaidi.

“Wanapobaini  maeneo hatari wakati wakiwasaka watu hao, wanalazimika kuliweka sawa kwanza kabla ya kuendelea. Kuna kamati nyingine ya wataalam ambayo hutoa taarifa kuhusu usalama kwa waokoaji,” amesema.

Julai 14, 2018 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alitembelea mgodi huo kujionea maendeleo ya uokoaji na kubainisha kuwa endapo uokoaji huo utashindikana na ikadhihirika wachimbaji hao wamefariki dunia, shimo hilo lifungwe.

 

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz