Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku tano ngumu za usafiri Moshi-Dar, wanafunzi walia

35013 Pic+usafiri Tatizo la usafiri katika Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Tatizo la usafiri katika Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro limeingia siku ya tano, huku wanafunzi pamoja na wafanyakazi wanaorudi kwenye sehemu zao za kazi wakilizwa na uhaba wa mabasi.

Ingawa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), ilitoa vibali vya muda kwa mabasi madogo Desemba 2018, kwa ajili ya kusafirisha abiria katika sikukuu za mwisho wa mwaka mpya, lakini hali ya usafiri imeendelea kuwa ngumu mjini hapa.

Jana, Mwananchi lilishuhudia baadhi ya daladala zinazofanya safari kati ya Mbagala na Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam zikibeba abiria ili kuziba pengo la uhaba wa mabasi katika stendi hiyo, lakini bado wasafiri walikuwa wengi huku malalamiko yakizidi.

Vilio vya wasafiri

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi waliokuwa wakirudi Dar es Salaam kuendelea na masomo yao baada ya kumalizika kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka walilalamikia uhaba wa mabasi na kwa machache yaliyopatikana kutozwa nauli kubwa.

Mmoja wa wanafunzi hao, Jesca Kimario wa Shule ya Sekondari Makongo, aliliambia Mwananchi kuwa alifika stendi saa 12 asubuhi, lakini magari yaliyokuwa yakifika kutoka Arusha yalikuwa yamejaa na yaliyokuwa na nafasi chache yaligombaniwa huku nauli zikiwa kubwa.

“Niko hapa stendi muda mrefu, nimeletwa na mjomba wangu lakini magari hakuna, mengi yakija tunaambiwa yamejaa na nauli ziko juu sana, gari ya Sh28,500 tunaambiwa ni Sh35,000 hadi Sh40,000 ila tunaendelea kusubiri maana Jumatatu tunafungua shule,” alisema.

Jonas Kavishe, aliyekuwa anakwenda Dar es Salaam alisema alifika kituoni hapo tangu saa 11, lakini magari yalikuwa yakifika yamejaa ambapo aliambiwa kuwa Januari 10 ndipo atapata usafiri.

“Sijui nini kinachoendelea hapa stendi, nimekuja tangu alfajiri ili nisafiri nirudi zangu kazini, cha kushangaza naambiwa magari yamejaa hadi tarehe 10 mwezi huu ndio nitapata nafasi ya magari yanayorudi Dar es Salaam,” alisema Kavishe.

Wasafiri Moshi-Arusha

Vilevile, wasafiri waliokuwa wakitokea mjini Moshi kwenda Arusha walikumbwa na adha ya usafiri baada ya magari yaliyokuwa yakifanya safari kubadili na kuanza kwenda Dar es Salaam.

Onesmo Laanyuni aliyekuwa akielekea jijini Arusha aliliambia gazeti hili kuwa abiria wanapata shida baada ya magari yaliyokuwa yakibeba abiria kubadilisha safari zake jambo ambalo limesababisha wasafiri wa Arusha kupanda daladala kutokea Moshi badala ya mabasi madogo aina ya Coaster.

“Usafiri wa kwenda Arusha sasa hivi ni wa shida sana, mchana hapa stendi hapakaliki, watu tunagombania daladala kama hatuna akili nzuri, hebu Sumatra waangalie hili jambo maana tunateseka, usafiri wa shida tangu Januari imeanza,” alisema.

Utetezi wa Sumatra

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Mkoa wa Kilimanjaro, John’s Makwale alisema tatizo la usafiri kwenda Dar es Salaam ni la muda na litakwisha kwani wameruhusu mabasi madogo 10 kutoka Kilimanjaro kupeleka abiria jijini humo.

“Sisi (Sumatra) Mkoa wa Kilimanjaro tumetoa vibali 10 tu vya mabasi madogo kwa ajili ya kusafirisha abiria kutokana na msongamano ambao upo hapa stendi, hivyo watuvumilie hili tatizo ni la muda na litaisha kabisa,” alisema Makwale.



Chanzo: mwananchi.co.tz