Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 285 za Nondo uraiani zafikia tamati

Sat, 5 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kusimamishwa masomo kwa siku 285, hatimaye uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umemrudisha chuoni hapo aliyekuwa mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo.

Nondo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu chuoni hapo alisimamishwa masomo Machi 26 mwaka jana baada ya kukutwa ana kesi ya kujibu katika mashtaka aliyofunguliwa na Jamhuri ikiwamo kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa na kuibua taharuki kwa jamii.

Hata hivyo, Novemba 5 mwaka jana Mahamaka ya Hakimu Mkazi mkoani Iringa chini ya Hakimu Mfawidhi, Liad Chamshana ilitoa hukumu na kumwachia huru baada ya kutomkuta na hatia.

Baada ya kumalizika kwa kesi hiyo, uongozi UDSM ulikuwa haujamruhusu Nondo kuendelea na masomo hadi Januari 2 alipoandikiwa barua akielezwa anaruhusiwa kurudi chuoni ili kuendelea na masomo.

“Kama unavyojua Machi 26 mwaka jana ulisimamishwa masomo kutokana na makosa mbalimbali. Napenda kukujulisha makamu mkuu wa chuo Desemba 27 alikuthibitisha kuendelea na masomo kuanzia Januari 6 mwaka huu,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alipotafutwa na Mwananchi hakukiri wala kukataa juu ya barua hiyo akisema hayupo ofisini atafutwe Jumatatu.

Akizungumzia uamuzi huo, Nondo anayesomea mwaka wa tatu shahada ya sayansi ya siasa chuoni hapo alisema: “Namshukuru Mungu na uongozi wote wa chuo changu kwa kunirejesha kumalizia masomo yangu. Mungu awabariki sana kwa uamuzi huu wa hekima na busara.”



Chanzo: mwananchi.co.tz