Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 145 bado familia yamtafuta Idrissa Dar

42561 PIC+IDRISA Siku 145 bado familia yamtafuta Idrissa Dar

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mama mzazi wa Idrissa Ally (13), aliyetekwa kwa staili ya ‘kimafia’, Leila Kombe ameiomba Serikali, wadau, viongozi wa dini na wabunge kukemea pia vitendo vya utekaji wa watoto kwa sababu havina tofauti na wale wanaouawa nchini sasa.

Idrissa aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate alitekwa Septemba 26, mwaka jana saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake maeneo ya Tegeta, Masaiti jijini Dar es Salaam.

Mtoto huyo, ambaye hadi jana amefikisha siku 145 tangu atekwe, alichukuliwa na dereva mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST.

Mwanaume huyo aliyeshuka kwenye gari na kuwafukuza marafiki wa Idrissa, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na kumuingiza mlango wa nyuma wa gari lake na kuondoka.

Akizungumza na Mwananchi jana, Leila alisema Jeshi la Polisi lingefanya jitihada kuwasaka watekaji kama ilivyofanya kwa Njombe kuwasaka wauaji, huenda watoto waliotekwa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha wangepatikana au wahusika wangekamatwa.

“Naishukuru Serikali na taasisi zilizojitokeza kulaani na kuyapigia kelele mauaji haya na kuchukua hatua kuyadhibiti, lakini mwamko huo usiishie huko watusaidie na sisi tuliopoteza watoto wetu,” alisema Leila.

Hivi karibuni, jumla ya watoto wanane wa umri wa chini ya miaka 10 wameuawa na maiti zao kukutwa zikiwa zimenyofolewa baadhi ya viungo mkoani Njombe.

“Ni jambo zuri walilolifanya la kukemea vitendo hivyo na nawaunga mkono, lakini nawaomba nguvu hiyo itumike pia kwa watoto walioibiwa na kutekwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Wakifanya hivyo, itasaidia wanaofanya vitendo hivyo kuacha, hata watoto waliotekwa huenda wakaachiwa kwa kuwa Serikali itakuwa inaendesha msako dhidi yao,” alisema mama yake Idrissa.

Alisema bado hajakata tamaa ya kumtafuta mwanawe licha ya miezi mitano kupita bila ya kuonekana.

Alirudia wito wake kwa kuwaomba Watanzania kutoa ushirikiano watakaomuona Idrissa au kusikia taarifa zake.



Chanzo: mwananchi.co.tz